WALIMU SHINYANGA WAONYWA KUHUSU MICHANGO SHULENI,ATAKEYEKIUKA ATAKUWA HAJIPENDIAfisa elimu wa mkoa wa Shinyanga Mohamed Kahundi akizungumza kwenye kikao cha wadau wa elimu mkoa wa ShinyangaWalimu mkoani Shinyanga wametakiwa kutojihusisha na suala la michango shuleni ili wasiingize kwenye matatizo wanapoteleza majukumu yao katika serikali ya awamu ya tano.

Rai hiyo imetolewa juzi na afisa elimu wa mkoa wa Shinyanga Mohamed Kahundi wakati wa kikao cha wadau wa elimu mkoani humo kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa.

Kahundi alisema kwa mujibu wa waraka wa elimu uliotolewa wizarani,mwalimu hapaswi kusimamia suala la michango na wala haruhusiwi kutoa wazo la kuanzisha mchango katika shule badala yake wazo litoke kwa wazazi na walezi wa wanafunzi.

“Mwalimu mkuu asionekane anachanga mchango shuleni,wewe uwe wa mwisho,waite wazazi,ukijifanya unachangisha mchango ni sawa na kujitafutia balaa,epukeni kabisa atakayefanya hivyo yatakayomkuta shauri yake”,alieleza Kahundi.

Katika hatua nyingine Kahundi alisema ni marufuku kwa mwanafunzi kurudishwa nyumbani kwa sababu hajalipa mchango shuleni na atakayebainika kukiuka taratibu atachukuliwa hatua.

Aidha afisa elimu huyo aliwataka walimu kutumia vizuri fedha za ruzuku kutoka serikalini ili zisiwaingize kwenye matatizo kwani yeyote atakayefanya ubadhirifu wa pesa hizo atakuwa hajipendi.

“Mkoa huu umepangiwa kiasi cha shilingi bilioni 3.8 kutoka wizarani kwa ajili ya ruzuku shuleni ila kiasi kilichotolewa ni cha robo mwaka ambacho ni shilingi bilion 1.8 hivyo walimu nawaomba mzingatie matumizi ya hizi fedha kwa kuangalia mahitaji muhimu na sio kufanya udanganyifu na kila mwezi ni lazima kuwasilisha ripoti mkoani”,alieleza Kahundi.


Naye mkuu wa mkoa wa Shinyanga Ally Nassoro Rufunga alisema mkoa hautasita kuwachukulia hatua walimu na watendaji watakaotumia vibaya pesa za ruzuku na kuwataka kusimamia pesa hizo kwa uadilifu mkubwa.

Mkuu huyo wa mkoa pia aliagiza kila halmashauri ya wilaya katika mkoa huo kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula na uji shuleni na huku akisisitiza kuwa serikali itawachukulia hatua wazazi wanaokatisha masomo ya watoto wao kwa kuwaozesha.
Na Kadama Malunde-Malunde1 blog Shinyanga

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post