WABUNGE WA UKAWA WAANZA KUMTIKISA SPIKA WA BUNGE,WASUSIA UCHAGUZI WA VIONGOZI WA KAMATI ZA BUNGE, ZITTO KABWE APONDA




Wakati vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge vikitarajiwa kuanza leo kwa uteuzi wa wajumbe, wabunge wa upinzani tayari wameanza kwa kumtikisa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Job Ndugai, baada ya kususia uchaguzi wa wenyeviti wa kamati hizo.


Dalili za mgawanyiko kwenye kamati hizo zilianza kuonekana juzi, baada ya wabunge hao wa Kambi ya Upinzani kufanya kikao na kuweka msimamo wa kutaka kushirikishwa kwenye uteuzi wa wajumbe.


Kambi ya Upinzani ilisema inataka kushirikishwa katika hatua hiyo ikidai kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM), imekuwa ikiwapangia watu wa kuongoza kamati zinazosimamia mapato ya serikali ambazo kikanuni zipo chini yao.

Viongozi hao wa kambi ya upinzani walidai kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakipangiwa watu wa kuongoza Kamati ya Hesabu za Serikali za (PAC) na ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), ambazo kikanuni zinatakiwa kuongozwa na upinzani.

Baada ya Ofisi ya Bunge kutangaza majina ya wajumbe wa kamati, Kambi ya Upinzani Bungeni ilikutana na waandishi wa habari, lakini wakaahirisha kwa madai kuwa wamegundua kwamba orodha ya majina yaliyotoka, yana matatizo mengi zaidi.


“Tumegundua kwamba matatizo hayapo kwenye kamati ya PAC na LAAC tu, kwenye kamati nyingi kuna matatizo kwa hiyo kwa sasa viongozi wa kambi wanakutana kujadili na kuchambua taarifa iliyotolewa baadaye tutakutana na wabunge wote kisha kesho tutatoa msimamo wetu,” alisema Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, John Mnyika.


Baada ya kauli hiyo, Mnyika aliulizwa inakuwaje wao wanaendelea na vikao wakati wenzao wa CCM wakiwa kwenye uchaguzi:


“Siwezi kujibu chochote, neno lolote nitakalosema, nitaingilia hicho kinachojadiliwa na viongozi. Wewe subiri kwanza tumalize kikao, tutoke na msimamo wa pamoja na kesho tutawaeleza msimamo wetu,” alisema Mnyika.


Awali, kabla ya kutolewa kwa majina hayo, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Magdalena Sakaya, alisema kwa muda sasa wamekuwa wakichaguliwa watu wa kuongoza kamati hizo na CCM.


“Ni sawa na mtu anakupa kitu kwa mkono wa kushoto na kukunyang'anya kwa mkono wa kulia. Ndiyo maana tukataka tushirikishwe kuanzia wajumbe watakaokuwa kwenye kamati hizo,” alisema Sakaya ambaye ni Mbunge wa Kaliua mkoani Tabora.


Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Aprili 2013, inasema: “Wenyeviti wa Kamati za Bunge zinazosimamia matumizi ya fedha za Umma ambazo ni Kamati ya Hesabu za Serikali, Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa, watachaguliwa kutoka miongoni mwa wajumbe wa kamati hizo ambao wanatoka katika Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.”

==>Kauli ya Zitto Kabwe kupitia ukurasa wake wa Facebook
Kupitia ukurasa wake wa facebook, Zitto Kabwe ambaye bunge lililopita alikuwa mwenyekiti wa PAC ameandika;

"Kamati zote za Bunge zina hadhi sawa ndani ya Bunge. Kila mbunge ana haki ya kuwa kwenye kamati yeyote ile na hakuna mbunge bora zaidi ya mwingine.



"Kanuni zimeweka utaratibu wa uteuzi kwenye Kamati ikiwemo maombi ya mbunge, uzoefu na ujuzi wa eneo husika.


"Wanaolalamika leo upangaji wa Kamati ndio usiku wa kuamkia jana walimshinikiza Spika asiwapange mahasimu wao kisiasa kwenye Kamati wanazoona wao ni nyeti.


"Ni unafiki uliopitiliza unapojenga hoja ya uzoefu, chaguo la Mbunge na ujuzi wakati huo huo wenye vigezo vyote hivyo unawapiga vita kwa sababu za kisiasa

"Ni dhahiri kuwa mpangilio wa Kamati unajenga Bunge kibogoyo, Nilitahadharisha toka Bunge la 11 lilipoanza kwamba, "kuna dalili za Serikali kutaka kulidhibiti Bunge ( kumbukeni sarakasi za Tulia Ackson ambaye sasa ni Naibu Spika) . "


"Kiongozi unapokwenda kwa Spika kusema 'fulani asipangwe Kamati fulani kwa sababu atapata sifa' halafu ukataka 'nyumbu' wako ndio wapangwe huko ujue unaisadia Serikali kudogosha Bunge.


"Spika anapoamua Nyote, huyo usiyemtaka na nyumbu wako wasiende huko ujue amekudharau sana.

"Unapoona Viongozi wa Serikali wanahangaika kupanga Kamati za Bunge watakavyo wao ujue viongozi hao ni dhaifu, hawana nia njema na hawataki kuwajibishwa.


"Twendeni kwenye hizi hizi Kamati tulizopangiwa kuwafanyia kazi Watanzania. Twendeni tukaonyeshe kuwa Bunge litabaki Bunge tu na Wabunge tusikubali Bunge Kibogoyo. Ni lazima Bunge lidhibiti Serikali hata Serikali hiyo ikiwa inaongozwa na Malaika.


"Serikali ni chombo cha mabavu lazima idhibitiwe, na ndio kazi ya Bunge kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 63."


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527