Inatisha Sana!! SIMBA AUA BABA NA MTOTO,ALITAFUNA MTOTO NA KUBAKIZA KICHWA TU NA KUNYONYA DAMU YA BABA HADI KUFA


 
 
Mnyama Simba amevamia Kijiji cha Sitalike Tarafa ya Nsimbo Wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi na kuuwa watu wawili.
 
Waliouawa ni baba na mtoto wake ambapo simba huyo kula mtoto na kuacha kichwa huku akinyonya damu ya mzazi hadi kupoteza maisha.

Tukio la Simba huyo kuua watu wawili limetokea  jana majira ya saa kumi na moja alfajiri katika Kijiji hicho cha Sitalike .

Mwenyekiti wa Kijiji hicho Christopher Anjelo aliwaambia waandishi wa habari  waliouawa kuwa ni John Jeremia (45) na mwanae wa kiume mwenye umri wa miaka mitano .

Alisema siku ya tukio wanafamilia hao walikuwa wamelala ndani ya nyumba yao ndipo simba huyo jike alipovamia na kuingia ndani ya nyumba hiyo .

Alieleza baada ya Simba huyo kuingia ndani alimvamia baba wa mtoto huyo na kuanza kumnyonya damu hadi alipohakikisha amefariki dunia ndipo alipomwachia marehemu huyo.

Mwenyekiti huyo wa Kijiji alisema simba huyo baada ya kuona John Jeremia amemnyonya damu hadi kufa alihamia kwa mtoto wake na marehemu na kuanza kumshambulia na kisha alianza kumtafuna na kubakiza kichwa tu na kwenda nacho hadi kwenye kichaka kilichokuwa jirani na nyumba ya marehemu hao.

Alisema taarifa za simba kuua watu hao zilifika kwenye uongozi wa Kijiji hicho ambao nao walitoa taarifa kwa askari wa Hifadhi ya Taifa ya Katavi ambapo walianza kufanya msako wa kumsaka simba huyo kwa kushirikiana na wananchi wa Kijiji cha Sitalike.

Wakati wakifanya msako waliona nyayo za simba na walizifuata kule zilipoelekea na walipofika kwenye kichaka walimuona simba huyo akiwa amekaa na pembeni yake kukiwa na kichwa cha mtoto .

Mwenyekiti wa Kijiji alisema askari wa Hifadhi ya Katavi walimfyatulia simba huyo risasi lakini aliweza kuikwepa na kusogea mbele zaidi .

Hata hivyo waliendelea kumfuata kwa kushirikiana na wananchi ndipo Askari wa TANAPA walipofanikiwa kupiga risasi na kufa hapo hapo.

Alieleza baada ya Simba huyo kuwa ameuawa kwa kupigwa risasi baadhi ya wananchi waliomba wamchukue kama kitoweo cha mboga lakini askari wa TANAPA waliwakatalia na walimchukua simba huyo aliyekuwa amekufa na kwenda nae kwenye hifadhi yao kwa kile walichoeleza kuwa wanakwenda kumchoma moto kwa kutumia mafuta ya petroli.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi Dhahiri Kidavashari amethibitisha kuuawa kwa watu hao na Simba huyo aliyetokea kwenye Hifadhi ya mbuga ya Katavi .

Alisema ameisha peleka askari wake kwenda kuangalia eneo la tukio hilo na ametoa wito kwa wananchi kuacha kujenga makazi karibu na hifadhi ya Katavi.
 
Na Walter Mguluchuma-Malunde1 blog Katavi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post