ASKARI POLISI AUAWA KWA KUPIGWA RISASI AKIFANYA UJAMBAZI USIKU WA MANANE HUKO KATAVI



Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi Dhahiri Kidavashari
******
Askari wa Jeshi la Polisi wa Wilaya ya Mpanda Mkoa Katavi Pc H 305 Nobart Chacha(25) ameuawa kwa kupigwa Risasi kifuani na mgongoni wakati akiwa anataka kufanya ujambazi na kupora mali za mfanyabiashara wa madini.

Mauaji ya askari wa huyo wa jeshi la polisi yametokea jana  wa saa nane usiku katika Kijiji cha Ibindi Kata ya Machimboni Wilayani Mlele.

Diwani wa Kata ya Machimboni Raphael Kalinga aliwaambia Waandishi wa Habari kuwa askari Polisi huyo akiwa na kundi la majambazi wenzake ambao idadi yao hakufahamika walifika kijijini hapo kwa lengo la kumvamia na kumpora kwa kutumia mapanga na shoka mfanya biashara wa Madini ya dhahabu na mashine za kusaga aitwaye Daniel John.

Alisema baada ya kuwa wamefika nyumbani kwa mfanyabiashara huyo walivunja mlango wa mbele wa nyumba ya mfanya biashara huyo ambaye alikuwa amelala ndani ya chumba chake .

Majambazi hao baada ya kuvunja mlango waliingia ndani na mfanya biashara huyo aliwauliza kuwa wao ni akina nani na ndipo walipomwamuru kuwa asipige kelele na anyamaze kimya vinginevyo watamuua.

Diwani Kalinga ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimmbo alieleza ndipo Daniel John alipojiandaa na kuchukua bunduki yake ya Short Gun na kufyatua risasi ambayo ilimpiga askari polisi huyo katika sehemu ya kifuani na mgongoni na kufa hapo hapo .

Alisema majambazi wenzake ambao walikuwa na silaha za jadi baada ya kuona mwenzao kapigwa risasi na kufa waliamua kumbeba marehemu na kwenda kumtupa kichani umbali wa mita 200 kutoka kwenye eneo la tukio na kisha walitokomea kusiko julikana.

Wakazi wa Kijiji hicho walifika nyumbani kwa mfanyabiashara huyo na kukuta michirizi ya damu na ndipo walipoamua kuifuata iliko kuwa inaelekea.

Alisema wanakijiji waliendelea kuifuata michirizi ya damu na ndipo walipofika umbali wa mita 200 kutokea nyumbani kwa Daniel John waliona mwili wa askari polisi ambaye alikuwa tayari amefariki dunia na ndipo taarifa zilipotolewa kwa jeshi la polisi Wilaya ya Mpanda.

Polisi walifika kwenye eneo hilo baada ya muda mfupi na ndipo walimtambua marehemu kuwa ni askari polisi wa kituo cha polisi cha Wilaya ya Mpanda .

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi Dhahiri Kidavashari amethibitisha kutokea kwa tukio la askari huyo kuuwawa kwa kupigwa risasi wakati akiwa anataka kufanya ujambazi na kupora .

Alisema mwili wa marehemu bado umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda .

Kabla ya tukio hilo kulikuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi wa Mkoa wa Katavi waliokuwa wakiwatuhumu baadhi ya askari wa Jeshi la polisi kuhusika katika matukio mbalimbali yaliyakuwa yakitokea ya ujambazi na uporaji katika maeneo ya Mkoa wa Katavi.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII HAPA
Na Walter Mguluchuma-Malunde1 blog Katavi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527