ANGALIA PICHA-RAIS MAGUFULI ATUA KWA KISHINDO ARUSHA,AAHIDI KUKOMAA NA MAFISADI WOTE


Ngoma za asili zikiwa zinatumbuiza katika uwanja wa KIA mara baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kutua na ndege uwanjani hapo








Baadhi ya wananchi waliojitokeza barabarani kumlaki Magufuli


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema kuwa nchi ya Tanzania ni tajiri na ina rasilimali nyingi ,ila baadhi ya matajiri ambao ni mafisadi ndio wanasababisha nchi yetu kuonekana maskini hivyo ameahidi kula nao sahani moja.


Aliyasema hayo leo wakati akiongea na wananchi wa mkoa wa Arusha waliojitokeza barabarani kumpokea huku wakimuomba aendelee kutumbua majipu.

Alisema kuwa nchi ya Tanzania ina rasilimali nyingi ila kuna baadhi ya matajiri ambao wanapenda kujilimbikizia fedha wamekuwa wakifanya ufisadi na kusababisha baadhi ya wananchi kuendelea kuwa maskini pamoja na nchi yetu kuonekana maskini .

“Nasema hivi kuanzia sasa nipo tayari kulala mbele na mafisadi wote na pia nawapa onyo kali wale walimu ambao bado wanatoza ada mashuleni iwapo nitagundua mwalimu yeyote anaetoza Hela naahidi hivi nitalala naye mbale ,na katika hili sitalifanyia masihara hata kidogo”,alisema Magufuli


Aidha aliwaambia wananchi kuwa kuanzia sasa elimu ni bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari na serikali imeshaweka mipango hiyo tayari na imeanza kutumika.


Magufuli aliwasihi wananchi wa mkoa wa Arusha na Tanzania kwa ujumla kuendelea kufanya kazi na kusema kuwa wakati wa kampeni umeisha , mambo ya siasa yameisha sasa hivi ni wakati wa kufanya kazi tu na sio kitu kingine.


“Nasema hivi sasa hivi ni wakati wa kufanya kazi kama nitaendelea kutumbua majipu kila mahali na sitawaonea huruma mtu yeyote mimi kazi yangu kubwa ni kufanya kazi tu na wananchi napenda kuwambia fanyeni kazi kwani hapa ni kazi tu”,alisema Magufuli.



Alisema yote aliyoyaahidi kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha na watanzania kwa ujumla ikiwemo ujenzi wa barabara za Arusha, kulipa fidia za wananchi na kufuta ada ya shule za msingi na sekondari yanatekelezwa. 
 
Dkt. Magufuli ametoa wito kwa watanzania kumuombea ili aendelee kuwashughulikia wote wanaofanya ubadhilifu wa fedha za umma kupitia kampeni yake ya kutumbua majipu.


Rais Magufuli amesisitiza kuwa serikali yake haitawabagua watanzania kwa dini zao wala makabila yao na wala haitawabagua kwa milengo ya vyama vyao na kanda zao na kuwataka watanzania wote kuiweka mbele Tanzania na kushirikiana kuiendeleza.



Rais magufuli alipokelewa na mamia ya wananchi mbalimbali ambao walijitokeza barabarani ambapo pindi tu alipotoka katika kiwanja cha KIA wananchi walikuwa wemejitokeza wengi mpaka ikamlazimu kufika katika baadhi ya maeneo na msafara wake kusimama ili wananchi waongee naye,sehemu ambazo aliweza kusimama ni pamoja na Kikatiti ,Usa River pamoja na Tengeru .
 Na Woinde Shizza-Arusha

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post