MWILI WA ASKARI ALIYEUAWA KWA KUPIGWA RISASI NA POLISI MWENZAKE WAAGWA JIJINI MWANZA, MWILI WA ALIYEUA HAUJAAGWAMkuu wa wilaya ya Nyamagana Baraka Konisaga amewaongoza askari na maofisa wa jeshi la polisi mkoani Mwanza kuaga mwili wa askari Polisi PC Petro Matiko wa kituo kikuu cha polisi jijini Mwanza, aliyeuawa kwa kupigwa risasi na askari mwenzake PC Daud Masunga kwenye lindo la benki ya Posta Tanzania tawi la Pamba. 
 
 
Akiwasilisha salamu za rambirambi kwa mkuu wa jeshi la polisi nchini (IGP) Ernest Mangu kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Mwanza, mkuu huyo wa wilaya ya Nyamagana ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama amesema kwamba kifo cha askari huyo kimekuja wakati ambao haukustahili kwani alikuwa ni tegemeo kubwa kwa taifa na familia yake.

Afisa mnadhimu wa jeshi la polisi mkoa wa Mwanza Japhet Lusingu ametoa pole kwa familia ya marehemu, sambamba na jeshi hilo mkoani hapa kutoa ubani wa shilingi milioni moja kwa baba mzazi wa marehemu PC Petro Matiko, huku mkuu wa kituo cha polisi Nyakato mratibu msaidizi Almachius Muchunguzi akisoma wasifu wa marehemu aliyezaliwa machi 25 mwaka 1989 katika kijiji cha Nkende wilaya ya Tarime mkoani Mara.

Shughuli ya kuaga mwili wa marehemu H.5950 PC Petro Matiko imetanguliwa na ibada ya mazishi iliyoongozwa na katekista wa kanisa katoliki Kigango cha Mabatini Bw. Elias Philipo Sajembe.

Mwili wa askari PC Daud Masunga Elisha haukuweza kuagwa kutokana na sababu ambazo hazikuwekwa bayana na uongozi wa jeshi la polisi mkoani Mwanza.
Via>>ITV

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527