MGANGA WA JADI MBARONI KWA KUKUTWA NA NYARA ZA SERIKALI...YAMO MAINI YA SWALA,NGOZI YA PAKA PORI,SIMBA ...

MGANGA wa Jadi aliyefahamika kwa jina la Vitus Chomba(42) mkazi wa Sumbawanga mjini mkoani Rukwa anashikiliwa na polisi wa wilaya ya Mlele mkoani Katavi baada ya kukutwa na nyara za serikali kinyume cha sheria.


Habari za uhakika kutoka eneo la tukio zinaeleza kwamba mganga huyo alikamatwa Desemba 27 saa 1 usiku, baada ya wakazi wa eneo alilokuwa akiishi kumtilia shaka kutokana na kukutana na watu kwa siri wakati yeye ni mgeni katika eneo hilo.

Akizungumzia tukio hilo afisa mtendaji wa kata ya Nsekwa wilayani Mlele mkoani Katavi Amos Ngozi alisema alipokea taarifa kutoka kwa wakazi wa kata hiyo wakieleza kuwa kuna mtu ambaye amekuwa akikutana kwa siri kubwa na baadhi ya wakazi wa kata hiyo hali iliyosababisha hofu kwa baadhi ya wananchi.

Alisema baada ya taarifa hizo alitoa taarifa polisi ambapo kwa kushirikiana na polisi hao walivamia katika nyumba anayoishi mganga huyo na kuanza kuifanyia upekuzi na katika beji lake la nguo walikuta kuna Ngozi ya simba, maini ya Swala pamoja na ngozi ya paka pori.

Mtendaji huyo wa kata alisema vitu vingine walivyokutwa navyo ni nyama ya Sungura, kwato za pundamilia pamoja na mkia wa nyati ambapo vyote thamani yake bado haijafahamika, vinavyodaiwa kutumia kwa ajili ya shughuli zake za uganga wa jadi na hutumia kwa ajili ya kutibu ama kuroga kutokana na huduma anayohitaji mteja wake.

Alisema mganga huyo alifika katika kijiji cha Inyonga wilayani humo kwalengo la kufuata wateja wake ambao walikuwa wamemuita awatibu na kuwafanyia zindiko pia kutafuta vitu ambavyo atavitumia katika kutengeneza dawa ambazo anatumia kutibia wateja wake.

Hata hivyo, mtendaji Ngozi alisema mganga huyo alichukuliwa na polisi na kushikiliwa katika kituo cha polisi kutokana na kukutwa akiwa na nyara za serikali, kosa la kufanya tiba za jadi wakati hana kibali cha kufanya kazi hiyo.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi mkoa huo, Dhahiri Kidavashari alikiri kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo na bado anahojiwa na polisi ili hatua zaidi za kisheria ziweze kuchukuliwa ikiwa pamoja na kufikishwa mahakamani.


Na Walter Mguluchuma-Malunde1 blog Katavi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527