WAZIRI MZIGO WA JK, AONESHA MAKUCHA KWA MAGUFULI...AFICHUA KISA CHA KUITWA WAZIRI MZIGO






Rais, Dk. John Magufuli, akimwapisha, Prof. Jumanne Magembe, kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Ikulu, jijini Dar es Salaam jana. Picha : Halima Kambi


Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, aliyeapishwa jana kushika wadhifa huo na Rais Dk. John Magufuli, amefunguka na kueleza sababu za kuitwa Waziri ‘mzigo’ wakati akiwa Wizara ya Maji, akitokea Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika.

Novemba 24,mwaka 2013, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, akiwa kwenye ziara za kuimarisha na kukagua Ilani ya chama hicho mkoani Ruvuma, kabla ya kuanza kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, alikutana na malalamiko ya wananchi juu ya uzembe wa mawaziri waliokuwa kwenye Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, waliowaita ‘mizigo’.

Mawaziri wengine waliotajwa kuwa mizigo ni Dk. Shukuru Kawambwa (Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi), Christropher Chiza (Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika) na Naibu wake

Akijibu tuhuma hizo baada ya kupenya kwenye Baraza la Mawaziri la Rais Dk. Magufuli, tofauti na watu wengi walivyodhani kutokana kashfa hiyo, Profesa Maghembe alisema waliomtaja kuwa ni mzigo ni majangili waliokuwa wanawinda wanyama na waandishi waliokuwa wanaandika na kulipwa na majangili.
“Wanaosema Waziri Maghembe ni mzigo hawajui na hawajafanya utafiti na usipofanya utafiti, huna haki ya kuzungumza, na wafikishieni taarifa Maghembe amerudi tena,” alisema.

Alisema mwaka 2007 akiwa Wizara ya Maliasili na Utalii, katika kipindi hicho, alifanya kazi kubwa ya kuhakikisha katika sekta ya uwindaji wanaongeza mapato ya serikali kuanzia Dola milioni saba zilizokuwa zinapatikana hadi kufikia Dola milioni 70 na kwa msingi huo, siyo mzigo.

Alisema pia walikuwa wakifanya kazi ya kukamata watu wanaosafirisha magogo kwenda nje ya nchi na kuongeza pato la taifa katika sekta ya misitu.

“Nashangaa hawa wanaoniita mimi ni mzigo, ningewezaje kufanya kazi hizi,” alisema Profesa Maghembe.

Alisema kwenye sekta ya maji aliyotoka, serikali ya awamu iliyopita, kulikuwa na Matojeo Makubwa Sasa (BRN), wizara yake ilifanyiwa tathmini na viongozi wakuu wanne wakiongozwa na Rais wa Botwana, Ian Khama, na kubaini kuwa wizara hiyo inaongoza.

“Hii wizara niliyotoka juzi ilifanyiwa tathmini na watu mashuhuri ambao walibaini wizara yangu inaongoza kati ya wizara sita zilizokuwa kwenye mpango wa BRN. Sasa unaniitaje mimi ni mzigo?,” alihoji Profesa Maghembe.

CHANZO: NIPASHE

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527