NOAH YATUMBUKIA MTONI NA KUUA WATU WATATU HUKO KATAVI



Picha haihusiani na habari hapa chini


WATU watatu wamekufa maji siku ya mkesha wa sikukuu ya Krismasi baada ya gari aina ya Noah walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kutumbukia mtoni.


Gari hilo la abiria lilikuwa likisafiri kutokana kijiji cha Muze wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa likielekea katika kijiji cha Majimoto wilayani Mlele mkoani Katavi.


Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga, Kalolo Joseph Ntila alisema kuwa tukio hilo lilitokea Desemba 24 saa 4:20 usiku ambapo gari hilo likiwa na abiria saba lilipoacha njia na kutumbukia katika mto huo.


Alisema kuwa baada ya gari hilo kutumbukia kwenye mto Kilambo ambapo baadhi ya abiria walifanya jitihada za kujiokoa ambapo walifanikiwa kutoka huku wanawake wawili na mtoto mdogo mmoja walishindwa kutoka ndani ya gari hilo na kufa maji wakiwa ndani ya gari hilo.


Ntila ambaye ni Diwani wa Kata ya Muze, alisema kuwa baada ya abiria hao kutoka walijitahidi kutoa msaada kwa watu waliokuwa wamebaki ndani ya gari hilo lakini hawakufanikiwa kutokana na maji mengi na walipofanikiwa waliwatoa wakiwa wamefariki dunia.

Alisema watu hao bado hawajafahamika majina yao lakini miili ya marehemu hiyo ilipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika kituo cha afya cha Muze kwaajili ya kusubiri kutambuliwa ili ndugu zao wakafanye maziko ya watu hao.


Diwani huyo aliongeza kwamba eneo hilo ambalo ajali hiyo imetokea si nzuri hasa nyakati hizi za masika pindi mvua zinaponyesha kumekuwa na utelezi hali iliyosababisha gari hilo kuteleza na kutumbukia mtoni.

Kamanda wa polisi mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo, na kutaka madereva wanaofanya safari kupitia barabara hiyo kuwa waangalifu katika nyakati hizi za masika kwani kutokana uharibifu mkubwa wa barabara kwenye eneo hilo.

Na Walter Mguluchuma-Malunde1 blog Katavi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527