Noma!! BEI YA MAJI YAPANDISHWA KINYEMELA MANISPAA YA SHINYANGA....WANANCHI WAIJIA JUU SHUWASSA


Sehemu ya mitambo ya kusafisha maji yanatoka katika bwawa la Ning'wa lililopo katika manispaa ya Shinyanga


Wakazi wa manispaa ya Shinyanga wameilalamikia Mamlaka ya Maji na usafi wa mazingira (SHUWASA) mjini Shinyanga kwa kupandisha bei ya maji, hali ambayo imesababisha washindwe kumudu gharama hizo na kuanza kutumia maji ya kwenye visima ambayo siyo safi na salama.

Wakizungumza na waandishi wa habari wiki iliyopita kwa nyakati tofauti baadhi ya wakazi hao wa Shinyanga mjini walisema wanasikitishwa na mamlaka hiyo ya maji kwa kupandisha bei kila mara na hivyo kuingiwa na wasiwasi wa kurudi kama zamani kutumia maji machafu ambayo siyo salama kwa afya ya binadamu.

Baadhi ya wananchi hao Ester John na Stanslaus Kulwa walisema Mamlaka hiyo (SHUWASA) ,imekuwa ikipandisha bei ya maji kinyemela na hivyo kuona haina umuhimu wa kuwa na mradi huo wa maji ya ziwa Victoria kutokana na kuwa na gharama kubwa ni bora kurudi kutumia maji ya bwawa la Ning’wa.

“Mwezi Oktoba nililipa bili ya maji Shilingi 14,000, lakini mwezi Novemba imekuja bili ya maji mara mbili yake Shilingi 26,000 na matumizi ni yale yale, lakini nilipo fuatilia SHUWASA nikaambiwa bei ya maji imepanda,” alisema John.

“Hata kama bei ya maji inapanda inatakiwa wananchi watarifiwe lakini siyo kujipandishia kinyemela au ndiyo tunarudisha gharama za uchaguzi, nchi hii mbona imejaa ubabe, kila kitu huwa kinafuata utaratibu na siyo kukurupuka tu na kuamka kujipandishia bei’,aliongeza Kulwa.

Naye kaimu mkurugenzi wa mamlaka hiyo ya Maji (SHUWASA), Flaviana Kifizi alikiri kupanda kwa bei hiyo ya maji, huku akibainisha sababu zake ni kutokana na kupanda kwa gharama za uendeshaji wa mamlaka hiyo.

Kifizi alitaja bei mpya ya maji iliyopanda kuwa unit moja itatozwa Shilingi 1,000, ambapo hapo awali mwezi uliopita ilikuwa shilingi 790, huku akifafanua kuwa bei hiyo ya maji itakuwa inapanda kila wakati ikitegemea na gharama hizo za uendeshaji wa mamlaka hiyo, na kuwataka wananchi wasihusishe suala hilo na uchaguzi.

Hata hivyo katika kipindi cha Kampeni wagombea ubunge na udiwani wa vyama vyote mjini Shinyanga ,walieleza kukerwa na bei kubwa ya Maji kutoka (SHUWASA), huku wakiahidi wakiingia madarakani watalishughulikia tatizo hilo ambalo limeonekana kero kwa wananchi wa mji huo.

Na Marco Maduhu- Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post