LOWASSA AIBUKIA KAHAMA KWA WAHANGA WA MGODI WALIOISHI KWA KULA MENDE NA VYURA SIKU 41 ARDHINI




Mgombea urais kwa tiketi ya CHADEMA Edward Lowassa leo ametoa shilingi Milioni 2 kwa wahanga waliookolewa katika mgodi wa Nyangalata wanaopatiwa matibabu katika hospitali ya halmashauri ya mji wa Kahama mkoani Shinyanga.





Akikabidhi fedha hizo kwa wahanga hao, Lowassa amesema ametoa fedha hizo kama msaada ili ziwasaidie kwa matibabu kwa muda wote watakapokuwa hospitalini hapo, ambapo kila mmoja amepatiwa shilingi laki tano.



Mmoja wa wahanga hao, Joseph Burule amesema kitendo cha Lowassa kuwatembelea hospitalini hapo kimewapa faraja kubwa, kwani tangu waokolewe na kuanza kupatiwa matibabu hakuna kiongozi mkubwa aliyefika kuwajulia hali pamoja na kuwapa pole.



Burule amesema kitendo hicho kinatakiwa kuwa mfano wa kuigwa kwa viongozi pindi linapotokea jambo la kusikitisha kama hilo, na kusema kuwa fedha hizo zitawasaidia kujikimu hospitalini hapo.



Kwa upande wake Mbunge wa viti maalumu Mkoa wa Shinyanga kupitia CHADEMA Salome Makamba amewaambia wananchi waliojitoza kumsabahi Lowassa kuwa, Lowassa amekuja kuwapa pole wahanga hao na hakuja kwa masuala ya kisiasa.



Novemba 15, 2015 wahanga 5 kati ya 6 waliofukiwa na kifusi katika machimbo ya nyangalata wilayani kahama waliopolewa wakiwa hai baada ya kukaa ndani ya mashimo kwa siku 41, ambapo jana mmoja kati yao amefariki dunia. 


Ni hivi karibuni baada ya kuokolewa mmoja wa wahanga hao alikaririwa akimuulizia Lowassa kama alishinda urais Tanzania kwenye uchaguzi na baada ya kuambiwa hakushinda alikosa raha.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527