LOWASSA ACHARUKA : POLISI WASIPOCHUKUA HATUA KWA WALIOMUUA MAWAZO TUTACHUKUA HATUA WENYEWE



 
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimelitaka jeshi la polisi kuwachukulia hatua watuhumiwa wanaodaiwa kumuua aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo, likishindwa kufanya hivyo, chama kitachukua hatua chenyewe.

LOWASSA
Akitoa salamu za rambirambi katika ibada ya kuuaga mwili wa Mawazo katika uwanja wa Furahisha jijini Mwanza, aliyekuwa mgombea wa urais kupitia Chadema na kuungwa mkono na vyama vya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, alisema polisi wasipochukua hatua kwa waliomuua mwenyekiti huyo, watachukua hatua wenyewe.

“Polisi wanafanya mambo yao ki-imra-imra, kwani magari ya washawasha yaliyonunuliwa kwa dola za Kimarekani milioni 282, hawana namna ya kuyatumia hivyo kuamua kuwachokoza wananchi ili waweze kuyatumia, sasa inabidi wachukue hatua kwa waliomuua Mawazo ama watachukua hatu wenyewe, “alisema.

Alisema baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza kutoa haki kwa familia na chama hicho kumuaga Mawazo, imeonekana jeshi la polisi halina intelijensia wanayodai wanafanya.

Lowassa alisema hukumu ya Jaji Lameck Mlacha wa Mahakama Kuu, iwe somo kwa polisi wa Tanzania kutokana na kujawa wivu usiofahamika.

MBOWE
Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, alisema chama hicho kinajiandaa kumfungulia mashitaka ya madai Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo, baada ya kuweka zuio la mwili wa Mawazo kutoagwa jijini Mwanza hadi Mahakama Kuu ilipotupilia mbali zuio hilo.

“Kamanda Mkumbo lazima alipe gharama zote za siku nane za kumweka Lowassa, Sumaye, Mbowe na wabunge zaidi ya 50 jijini Mwanza wakisubiri mahakama itende haki na hatimaye kushinda kesi, ”alisema mwenyekiti Mbowe.

Alisema haki imepatikana mahakamani na kuwaumbua polisi.
“Wananchi wamechoka kuuliwa kama ilivyotokea kwa wafuasi wa Chadema tangu mwaka 2011 mpaka sasa wakati huu wa Mawazo tumechoka kufa, mwenye akili na afahamu,ö alisema Mbowe.

Hata hivyo, alisema wapo baadhi ya askari polisi wema na wenye kutekeleza weledi wa kazi zao kiufasaha, lakini wapo ambao hawafai kuwatumikia na kuwaongoza wananchi.

Aliwashukuru watu waliojitolea kuisaidia familia ya marehemu Mawazo hasa mtoto wake Precious Mawazo (9) anayesoma darasa la nne akiwamo Lowassa pamoja na wabunge 113 wanaotoka vyama vya Ukawa, kwa kila mmoja kujitolea Sh. 300,000 na kupatikana milioni 36.

SUMAYE
Waziri Mkuu mstaafu wa serikali ya awamu ya tatu, Frederick Sumaye, alisema Tanzania awali ilikuwa inasifiwa kwa amani na utulivu, lakini inawaua watu wanaodai haki.

“Hii ni kama ilivyokuwa Afrika Kusini wakati wa utawala wa Makaburu, mpigania haki Steve Bicco, aliuawa kama alivyouawa Mawazo, lakini mwisho wake makaburu hao walitoa haki kwa waliowengi licha ya kuwa na bunduki na polisi wengi kuliko kwetu, “alisema Sumaye.

Sumaye alisema marehemu Mawazo alikuwa akidai haki majukwaani, lakini watu waliotaka kudaiwa haki waliamua kumuua huku vyombo vya dola vikipindapinda ili haki isipatikane kwa amani.

MTOTO WA MAWAZO
Mtoto wa marehemu Mawazo, Precious (9), alisema waliomuua baba yake hawajakatisha ndoto yake ya kuwa mwanasiasa kwani siku moja atakuwa mwanasiasa mkubwa.

“Wakati wa uhai wa baba, ndoto yangu ilikuwa niwe mwanasiasa, lakini nitaendelea na hiyo ndoto hadi niwe mwanasiasa mkubwa nchini katuacha na mdogo wangu akiwa na miaka miwili tunaamini Mungu atatusaidia, “alisema Precious.

LEMA
Aliyekuwa mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema, akitoa salamu za rambirambi uwanjani hapo, alisema marehemu Mawazo alikuwa rafiki yake wa damu tangu akiwa jijini Arusha na kumshawishi kuingia kwenye siasa, lakini aliuawa kinyama na watu wasiopenda haki.

Lema alisema ukimya wa wananchi katika mauaji wanayofanyiwa, si uoga bali unatokana na uchungu walionao, kwani wauaji wakiwa huru hakuna atakayekuwa salama.

MCHUNGAJI SWAI
Mchungaji Bernard Swai wa kanisa la Winners jijini Mwanza, akihubiri katika misa ya kumuaga, alisema wanadamu hawajumbwa na Mungu kwa ajili ya kuuana bali kupendana.

“Lazima wanadamu wajiulize kwanini vijana wengi wanatumiwa ili kuwaua wengine, tunaiomba serikali iliyopo madarakani isimamie na kukomesha kabisa mauaji yasiyo na hatia, “alisema Mchungaji Swai.

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527