BAADA YA RAIS MAGUFULI KUTUMBUA MAJIPU YA BANDARINI...TAYARI WATUHUMIWA 12 WAMETIWA MBARONI




Kufuatia agizo la Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa la kuwataka watuhumiwa wa wizi wa makontena 329 katika bandari ya Dar es salaam kuchukuliwa hatua na Jeshi la Polisi, tayari Jeshi hilo limewashikilia watuhumiwa kumi na mbili wanaohusika na wizi huo.


Akiongea na waandishi wa habari leo Jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (CP) Diwani Athumani amesema kuwa, uchunguzi unaofanywa na wataalamu waliobobea katika makosa ya uhalifu wa kifedha umeweza kuwabaini watu kumi na mbili ambao wamehusika na wizi huo.


“Kati ya watuhumiwa hao kumi na mbili, watano wanashikiliwa na Jeshi la Polisi na saba bado wapo katika upepelezi na upelelezi utakapokamilika watafikishwa mahakamani,” alisema Kamanda Athumani.


Wanaoshikiliwa kutokana na tuhuma mbalimbali ni Kamishna wa Idara ya Forodha na Ushuru TRA Bw. Tiagi Masamaki, Meneja Kitengo cha Huduma za Ushuru na Bi. Habib Mponezia, Msimamizi Mkuu wa Kitengo cha Ushuru wa Forodha.


Watuhumiwa wengine ni pamoja na Bi. Eliaichi Mrema, Msimamizi Kitengo cha Mawasiliano ya Kompyuta Bw. Haroun Mpande na Mchambuzi Mwandamizi wa Masuala ya Biashara Bw. Hamis Omary.


Aidha Kamanda Athumani amewaomba wananchi wenye taarifa za ubadhilifu wa mali za Umma kuendelea kulisaidia Jeshi la Polisi katika kutekeleza majukumu yake.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527