Kadhalika, alisema ni vyema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) na
mamlaka za serikali iliyopo madarakani kuheshimu maamuzi ya wananchi
yatakayotokana na kura watakazopiga kwenye uchaguzi mkuu Jumapili ijayo,
kwani kinyume chake ni kuhatarisha amani iliyopo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana baada ya kutoa heshima za
mwisho kwa mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Dk. Emmanuel
Makaidi wa chama cha National League for Democracy (NLD) aliyefariki
dunia wiki iliyopita, Mbowe alisema watakubali matokeo ikiwa mchakato
wote wa uchaguzi utakuwa huru, wa haki na usiokuwa na chembe ya mizengwe
katika kila hatua.
Chadema na vyama vingine vinavyounda Ukawa vya Chama cha Wananchi
(Cuf), NCCR-Mageuzi na NLD, vimemsimamisha waziri mkuu wa zamani, Edward
Lowassa kuwa mgombea wao wa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, huku pia wakishirikiana kusimamisha wagombea wa nafasi za
ubunge, udiwani na uwakilishi.
Akieleza zaidi, Mbowe aliyekuwa akijibu swali aliloulizwa na
waandishi kuhusu namna walivyojiandaa kupokea matokeo baada ya uchaguzi
mkuu Jumapili ijayo, alisema Ukawa itakuwa tayari kupokea matokeo
yatakayotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ikiwa wataridhika
kuwa hatua zote za kisheria na haki za mchakato wa uchaguzi huo kuanzia
katika kampeni hadi upigaji kura zimezingatiwa ipasavyo.
Aliongeza kuwa kinyume chake, wao (Ukawa) hawatakuwa tayari kupokea matokeo yatokanayo na hila za namna yoyote ile.
Akifafanua, Mbowe alisema Ukawa haiwezi kukataa matokeo kwa sababu
ya kushindwa katika uchaguzi, bali wanachoangalia ni kuzingatiwa kwa
haki, sheria na uwazi katika hatua zote za mchakato wa uchaguzi huo.
“Kupokea matokeo ni mchakato ambao unaanzia katika hatua za
kampeni, upigaji kura hadi wakati matokeo yanatangazwa. Siwezi kusema
eti tutakataa matokeo kwa sababu tu Nec imetangaza halafu tukaonekana
tumeshindwa… la hasha. Bali tutapokea matokeo kama haki, uwazi, sheria
na taratibu nyingine zimezingatiwa mpaka kupatikana kwa matokeo,”
alisema Mbowe na kuongeza:
“Sisi Chadema na Ukawa tunaamini kwamba wananchi watamchagua
kiongozi wanayemuamini. Lakini kama watu wengine wenye mamlaka ndani ya
nchi wakaamua kupindisha sheria na kupindisha maamuzi ya wananchi
kupitia sanduku la kura, kamwe hatutakubali matokeo hayo. Na hapo amani
tunayoihubiri inaweza kuwa ngumu ‘kui-control’ (kuidhibiti),” alisema.
Kuhusiana na mvutano juu ya wananchi kuondoka vituoni baada ya
kupiga kura na siyo kukaa mita 200 kutoka kwenye vituo vya kura, Mbowe
alisema msimao wao wa kulinda kura uko pale pale kwa kuwa wana amini
kuwa hiyo ni haki yao kisheria.
“Kura ni mali na kama hivyo ndivyo ni lazima tuilinde, tumepanga
kulinda kura zetu kwa amani na utulivu nje ya mita 200 kama sheria
inavyosema… tunaomba kila mtu na vyombo vya dola viheshimu,” alisema.
Aliongeza: “Kuhubiri amani bila haki ni kulishana upepo. Mamlaka
zote za taifa zina wajibu wa kuheshimu sheria za nchi na kuacha kutumia
mamlaka zao vibaya na bila vitisho. Kila mmoja akitekeleza wajibu wake
kwa misingi ya sheria, hiyo amani wala haitatafutwa, itapatikana tu.”
Mbali na Mbowe, wengine waliojitokeza katika shughuli ya kuuaga
mwili wa Dk. Makaidi ni Lowassa, Mgombea Mwenza wa Ukawa, Juma Duni
Haji, Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia wa NCCR-Mageuzi , Waziri
Mkuu Mstaafu aliyehamia kambi ya Ukawa, Frederick Sumaye, Kaimu Katibu
Mkuu wa Cuf, Twaha Tasilima, Katibu Mkuu wa NLD, Tozzy Matwanga na
Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula.
Wengine waliokuwapo ni Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, mgombea ubunge wa Jimbo la Kawe, Halima Mdee.
MZIRAY
Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Peter Kuga Mziray na Mwenyekiti wa Chadema Bara, Prof. Abdallah Safari.
Akitoa salamu zake, Mziray alisema viongozi wote wameupokea msiba huo kwa masikitiko makubwa.
Mbatia alisema Dk. Makaidi alikuwa kiongozi aliyeamini kwenye
mageuzi, mabadiliko na kuamini kuwa Tanzania bila CCM inawezekana.
MTOTO WA MAREHEMU
Mtoto wa Marehemu, Oscar Makaidi, alisema baba yake alifariki akiwa
katika harakati za kugombania Ubunge Jimbo la Masasi ili kuleta
mabadiliko na hivyo akawataka viongozi waliobaki kushirikiana kutimiza
ndoto ya marehemu baba yake aliyefariki Oktoba 15 katika Hospitali ya
Nyangao mkoani Lindi. Dk. Makaidi alizaliwa Masasi, Aprili 10, 1941 na
ameacha mjane na watoto kumi.
LOWASSA AITWA RAIS MSIBANI
Baada ya shughuli ya kuuaga mwili wa marehemu katika viwanja vya
Karimjee, mwili wa Dk. Makaidi ulipelekwa kwenye makaburi ya Sinza na
kuzikwa na mamia ya wananchi waliojitokeza.
Katika hatua isiyotarajiwa, baadhi ya wananchi walishindwa kuficha
mahaba yao kwa Lowassa katika eneo la makaburi na kujikuta
wakimshangilia wakati akiwasili na pia kuondoka, huku wakiimba kwa
kumwita ‘Rais, Rais, Rais!’.
Mwili wa marehemu Makaidi uliwasili katika makaburi ya Sinza saa
9:15 alasiri na baada ya kuwasili waombolezaji wengi walianza
kumshangilia Lowassa wakati akishuka kutoka kwenye gari alilokuwamo
kuelekea katika makaburi hayo, huku naye akiwapungia mkono.
Hata baada ya mazishi, Lowassa alishangiliwa vilevile kwa kuitwa
‘Rais’ wakati akiondoka baada ya yeye na viongozi wa Ukawa wakiwamo
Mbowe na Mbatia kuweka maua katika kaburi la Dk. Makaidi.
JAJI MKUU ATAKA MAHAKAMA IACHIWE SUALA LA MITA 200
Wakati Mbowe akisisitiza msimamo wa kuwataka wafuasi wa Ukawa
kutorudi nyumbani baada ya kupiga kura na badala yake kukaa umbali wa
mita 200 kutoka vituo vya kupigia kura ili kulinda kura zao, Jaji Mkuu
Othman Chande alikataa kuzungumzia suala hilo na badala yake kutaka
mahakama iachiwe ili itoe uamuzi wake kwa haki.
Jaji Chande aliyasema hayo jana wakati alipoulizwa na waandishi
baada ya kufungua mafunzo kwa majaji na Wasajili Mahakama Kuu Jijini Dar
es Salaam, juu ya wajibu wa mahakama katika uchaguzi mkuu na namna ya
kukabiliana na changamoto zilizopo katika kusimamia kesi za uchaguzi,
yaliyoandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC).
Tayari Mahakama Kuu imeshapanga majaji watatu kushughulikia suala
hilo lililoibua mvutano mkali hivi karibuni baina ya viongozi wa Ukawa
na wakuu wa Nec na Jeshi la Polisi. Kesi hiyo itaanza kunguruma rasmi
leo.
Katika hatua nyingine, Jaji Chande alikiri kuwa uchaguzi wa mwaka
huu ni wenye mchuano mkali na kwamba mahakama zimejiandaa kumaliza kesi
zitakazotokana na uchaguzi huo kabla ya miezi sita inayotajwa kisheria.
Alisema mwaka 2010 kulikuwa na kesi 44 za uchaguzi kwa ngazi za
Ubunge na kati yake, 17 zilikwenda hadi hatua ya mwisho baada ya
kutolewa ushahidi huku nyingine zikiisha katika hatua za awali.
“Ushindani ni mkali katika uchaguzi huu, tunatarajia kupokea kesi
nyingi za uchaguzi. Tumejiandaa kupokea, kusikiliza kwa haraka ili
kuwezesha wapigakura kujua mshindi halali ni yupi,” alisema.
Akieleza zaidi, alisema sheria imeweka wazi kuwa anayestahili kufungua kesi siyo mpigakura bali wagombea wenyewe.
Mratibu THRDC, Onesmo Olengurumwa, alisema wameshirikiana na Ofisi
ya Jaji Kiongozi kuandaa mafunzo hayo kwa kutambua kuwa ni wadau muhimu
katika kushughulikia kesi za uchaguzi ili kuwezesha haki kutendeka kwa
haraka
GOODLUCK JONATHAN AKIRI NGOMA NZITO CCM, UKAWA
Mkuu wa Jopo la Waangalizi kutoka Jumuiya ya Madola na aliyekuwa
Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan, amekiri kuwa uchaguzi wa mwaka huu
nchini Tanzania una ushindani mkali kutokana na namna vyama
vilivyojiandaa lakini akawataka wagombea wote wa nafasi za urais
kujiandaa kukubali matokeo kwa maslahi mapana ya taifa lao.
Wagombea wanaochuana kwa karibu ni, Dk. John Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Lowassa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam mara
baada ya kuwasili nchini, Jonathan aliyekubali kuondoka madarakani Mei
mwaka huu na kumpisha Muhammad Buhari baada ya kushindwa katika uchaguzi
mkuu nchini mwake, alisema katika uchaguzi wowote kuna kushinda na
kushindwa na hivyo wagombea wajiandae kwa matokeo yoyote ili kuiacha
nchi yao ikiwa salama.
Alisema ijapokuwa ushindani ni mkali, Jumuiya ya Madola inaamini
kuwa uchaguzi utakuwa huru na haki na kwamba imani yao kubwa ni Tanzania
kusimamia demokrasia iliyokuwapo wakati wote tangu ipatre uhuru wake
mwaka 1961.
Jonathan anaongeza jopo lenye waangalizi 14 kutoka mataifa mbalimbali yaliyo wanachama wa Jumuiya ya Madola
CHANZO:
NIPASHE
Social Plugin