Mgombea Ubunge jimbo la Shinyanga mjini Stephen Masele akizungumza katika moja ya mikutano yake ya kampeni-Picha na Kadama Malunde-Malunde1 blog |
########
Mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM katika jimbo la Shinyanga mjini, Stephen Masele (pichani) ametamba kuibuka na ushindi mkubwa kutokana na kuungwa mkono na wananchi wengi wakiwemo waliokuwa madiwani wa CHADEMA katika manispaa ya Shinyanga.
Masele alitoa kauli hiyo jana kwa nyakati tofauti alipokuwa akiwahutubia wakazi wa Shinyanga kwenye mikutano yake ya kampeni ya kuomba kura iliyofanyika katika kata za Ibinzamata na Ndala manispaa ya Shinyanga.
Akiwa katika viwanja vya kanisa la Anglikana kata ya Ndala, Masele aliwaomba wakazi wa kata hiyo bila kujali itikadi za vyama vyao wahakikishe Oktoba 25, mwaka huu wanamchagua kwa kura nyingi ili aendelee kuwa mbunge wao.
Alisema anaamini katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ameweza kutekeleza vyema ahadi alizozitoa kwa wananchi mwaka 2010 na kwamba ni vizuri wakamchagua tena ili aweze kuendeleza miradi mingi aliyoianzisha ikiwemo ujenzi wa viwanda saba vilivyosalia kujengwa kati ya 12 alivyokuwa ameahidi.
Masele ambaye pia ni Naibu waziri ofisi ya makamu wa Rais, alisema hivi sasa anaungwa mkono na waliokuwa madiwani kwa tiketi ya CHADEMA, George Kitalama na Zainabu Kheri kutokana na kuridhishwa kwao na kazi kubwa alizozifanya jimboni.
“Ndugu zangu tupo hapa kuwaombeni kura zenu zote mtupigie wagombea wa CCM, kwa urais mpigieni Dkt. John Magufuli, ubunge nipeni mimi (Masele) na udiwani kwa ndugu yetu Abel Kaholwe, msiangalie vyama, angalieni nimewafanyia nini, nawashukuru sana viongozi wa CHADEMA ambao sasa wanaoniunga mkono waziwazi” ,alisema Masele.
“Namshukuru sana dada yangu Zainabu Kheri kwa kuamua kujitoa waziwazi kuniunga mkono,wamechoshwa na mgombea wao kwa sababu ana kiburi,mjuaji,amajifanya yeye ndiyo amesoma kuliko wote,hana msaada hata kwa madiwani wake,wamechoshwa...Zainabu Heri Nakushukuru sana dada yangu...naomba uendelee hivyo hivyo kunisaida na waambie wanachadema wengine...tunachagua mtu safari hii hatuchagui Chama na mtu mwenyewe ni Masele.....",alisema Masele.
"Nimshukuru sana George Kitalama huyu ni katibu wa Chadema wilaya ya Shinyanga anayekaimu naye amechoshwa na ukiritimba wa mgombea wao....na yeye ameamua kususia kule Kitangiri ananisaidia kunipigia kampeni..anafanya kampeni mchana kweupe..kwa sababu amechoka..nawaomba na wana Ndala mlioko Chadema mnipigie kampeni,mnipigie kura ili chama chenu kipate akili kwa makosa kiliyofanya ya kuwanyanyasa na kuwadharau waliokuwa waliokijenga chama hiki...",aliongeza.
Hata hivyo wakiongea na Malunde1 blog kwa njia ya simu ya kiganjani wanachama hao wa CHADEMA walikanusha vikali madai ya kumuunga mkono mgombea huyo wa CCM na kueleza huenda ameishiwa na hoja za kuwaeleza wapiga kura wake baada ya kutofanikiwa kutekeleza kikamilifu ahadi alizokuwa amewaahidi mwaka 2010.
"Anachokifanya huyu mpinzani wetu ni kujitafutia tu umaarufu kupitia Makamanda wa Chadema,haiwezi kutokea hata siku moja tuumunge mkono..ameshaona muziki mnene wa Katambi ameanza kupoteza mwelekeo..ajiandae tu kung'oka",walisema.
“Nimesikia hizo habari kutoka kwa wanachama wetu wa kata ya Ibinzamata wametueleza jinsi huyo bwana anavyodai sisi tunamuunga mkono, ni muongo, ameishiwa hoja, hatuwezi kumuunga mkono mpinzani wetu mkubwa, na hivi tunavyoongea tupo kata ya Kolandoto kwenye mkutano wa kampeni za mgombea ubunge wetu Katambi,” alieleza Kitalama.
Kwa upande wake Zainabu Kheri aliyekuwa diwani wa viti maalumu kwa tiketi ya CHADEMA alikanusha madai ya Masele na kueleza kwamba inawezekana ameanza kuona dalili za kushindwa hapo Oktoba 25, mwaka huu baada ya kuona mgombea ubunge wa CHADEMA anaungwa mkono na wananchi wengi jimboni.
Na Suleiman Abeid na Kadama Malunde-Malunde1 blog
Social Plugin