WAZIRI MKUU PINDA AFUNGUKA ALIVYOKATWA URAIS CCM "TAMAA YANGU IKAISHIA KUWA RAIS WA FIKRA TU"
Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ambaye alianguka katika hatua za awali za mbio za urais ndani ya CCM, amesema ameishia kuwa “rais wa fikra”.


Pinda, ambaye amekuwa Waziri Mkuu kwa takriban miaka minane, hakuweza kuingia katika orodha ya makada watano ambao majina yao yalipelekwa Halmashauri Kuu kwa ajili ya kupata majina matatu ya kupelekwa Mkutano Mkuu kwa ajili ya kupata mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho tawala.


Baada ya mchakato huo kumalizika, mbunge huyo wa Katavi amekuwa kimya, lakini jana aliibuka na kuzungumzia mbio hizo zilizoacha majeraha kwenye chama hicho kikongwe.


Pinda alisema mchakato huo ulikuwa hauna kulala, wa haraka haraka, ambao uliisha kwa CCM kupata mgombea ambaye alimuelezea kuwa “ni chaguo la Mungu”.


Akizungumza baada ya kupokea taarifa fupi ya Mkoa wa Mbeya kuhitimisha maonyesho ya Nanenane jijini Mbeya, Pinda alisema alitamani sana kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania.


“Mimi ninaamini Mungu ndiye anayepanga kwani sikuzaliwa kuwa Waziri Mkuu wala kuwa Rais, lakini nilipangiwa uwaziri mkuu ambao nimefanya kazi hiyo hadi nimechoka,” alisema Pinda, ambaye alikuwa mmoja wa makada 42 wa CCM waliojitokeza kuwania ridhaa ya chama hicho kugombea urais.


“Baada ya mchakato ule, alipatikana mtu mahiri ambaye Mungu alimpanga, lakini tamaa yangu, ikaishia kuwa rais wa fikra tu.”


Alisema mchakato ulifanyika kwa kasi bila kulala na wakapatikana watano, mara watatu na hatimaye mmoja.


“Suala hilo halitakiwi kuwa sababu ya kugombana, kulaumiana na kutoana macho, kwani ni sawa na kugombana na Mungu,” alisema Pinda.


“Hata mimi nilitamani sana kuwa Rais, lakini sasa yamekwisha. Sina sababu ya kuwa na hasira au kuhama chama kwani haina tija na hasira ni hasara.


“Sina sababu ya kuhama chama, nitabaki CCM na baada ya Oktoba nitakuwa mkulima mzuri ambaye nitashirikiana na wenzangu kuendeleza nchi.” Pinda alisema mgombea wa CCM, Dk John Magufuli ni mzuri na kwamba Mungu atamsaidia kujua mahitaji mengine ya Taifa na Watanzania.


Alisema ana uhakika kwamba ifikapo mwaka 2025, hali ya umaskini katika kaya itakuwa imepungua.


Aliwataka wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na maofisa wote wa Serikali waliogombea urais, ubunge na udiwani ambao walishindwa katika kura mbalimbali, wakubali matokeo na wachape kazi bila kinyongo na kwamba Serikali ijayo itawafikiria kwa utendaji mzuri.


Awali, katika taarifa yake fupi, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro alisema yeye na viongozi wengine waliwania ubunge, lakini wameshindwa na wataendelea kuchapa kazi ya Serikali.


Kandoro alizungumzia utekelezaji wa maagizo mbalimbali aliyopewa na Waziri Mkuu likiwamo la kuwashughulikia wanaume waliowapa mimba wanafunzi wa sekondari na alisema watu 176 walikamatwa na 53 kati yao, kesi zipo mahakamani wakati wengine walifungwa na wengine uchunguzi unaendelea.


Kuhusu agizo la kuhakikisha wanawake wanapimwa ili kujua hali ya kansa mkoani Mbeya, alisema wanawake 7,241 walipimwa na 200 kati yao walionekana kuwa na saratani ya shingo kizazi.

Chanzo-Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post