RAIS KIKWETE AWAPIGA VIJEMBE UKAWA" HUO MWINGINE NI MOTO WA MABUA TU HAUWAKI UKADUMU",CCM ITASHINDARais Jakaya Kikwete amesema anaamini mgombea wa urais kupitia CCM, Dk John Magufuli ndiye atakayeshinda katika Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu, na kwamba vuguvuru la kisiasa linaloendelea hivi sasa ni moto wa mabua.


Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM alikuwa akihutubia watendaji wa Wizara ya Ujenzi na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo katika hafla ya kumuaga, iliyofanyika kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.


Kauli ya Rais Kikwete inaweza kutafsiriwa kuwa ni vijembe kwa vyama pinzani, hasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), vinavyoendelea na pilikapilika zake tangu kumpokea Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa aliyehamia Chadema kutoka CCM na kuteuliwa kuwania urais, huku nao wakitupia vijembe CCM.


“Sishangai chama chako kimekuteua kuwa mgombea wa urais wa chama hicho ambacho ndiyo chama changu na mimi ndiyo mwenyekiti wake, nina imani Mwenyezi Mungu akijalia, kazi iliyobakia tutaikamilisha kwa salama. Huo mwingine ni moto wa mabua tu, hauwaki ukadumu,” alisema Rais Kikwete na kushangiliwa na wahandisi hao.


Jina la Lowassa lilikatwa pamoja na wagombea wengine 38 wa CCM walioomba kuteuliwa kuwania urais kupitia chama hicho katika vikao vyake vya Halmashauri Kuu ya Taifa na Kamati Kuu, vilivyoketi makao makuu yake mjini Dodoma.


“Huwezi kulazimisha, hata ukilazimisha hayawi,” alisema Rais Kikwete na kuamsha shangwe nyingine uwanjani hapo huku akiwaambia: “Mtampata mwenzenu, inshallah;… ombi langu mpeni ushirikiano rais ajaye, kwani kutokana na kazi yenu nchi imefikia mahali pa kuanza ‘ku-take off.”


Kikwete aliyewasili uwanjani hapo saa 5:02 asubuhi na kuanza kupokea taarifa za utekelezaji za atendaji wakuu wa taasisi saba zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi katika miaka 10 inayomalizika, kabla ya Dk Magufuli kumkaribisha kutokana na utendaji wake, taifa likimpata Dk Magufuli litanufaika kwani ni kiongozi mzuri.


Rais Kikwete aliyetumia takriban dakika 47 kutoa hotuba ya kuwaaga wafanyakazi wa wizara hiyo, alimsifu na kumshukuru Dk Magufuli akimwelezea kuwa ni msikivu aliyefanya kazi nzuri, iliyomfanya alale usingizi usio na mawaa.


Vile vile, Rais alitumia muda huo kuwaeleza wananchi kuwa mara atakapotoka madarakani atakwenda kuishi kijijini kwake Msoga, wilayani Bagamoyo katika Mkoa wa Pwani na kwamba asingependa watu wamfuate fuate huko.


Alisema akirejea kijijini kwake atafuga ng’ombe na kulima mananasi kwa kuwa ana eneo la ekari 1000 lililopo katika jijini cha Kibindu alilopewa wakati akiwa mbunge wa Chalinze na kwamba akikaa kijiji atakuwa na utulivu wa kutosha hivyo wasimfuatefuate.


Tangu Lowassa aenguliwe katika kinyang’anyiro cha kuingia Ikulu kwa tiketi ya CCM na baadaye kujiunga na Chadema, kumekuwapo na vuguvugu la wanachama wengi wa CCM kukihama chama hicho na kumfuata.


Akiwahutubia mamia ya wafuasi wa Ukawa muda mfupi baada ya kuchukua fomu ya kugombea urais Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), makao makuu ya Chadema, Lowassa alisema rafike yake Kikwete ndiye aliyeharibu uchumi, lakini akasema asingetaka kutoa mashtaka bila kutoa takwimu.


“Wakati Rais Benjamini Mkapa anaondoka madarakani, bei ya sukari ilikuwa Sh650, leo ni Sh2, 300, kutoka 650 hadi 2,300 ameharibu uchumi, hajaharibu?” aliuliza na kujibiwa, “ameharibuuu.”


Magufuli


Akimkaribisha Rais Kikwete, Dk Magufuli katika hotuba yake iliyochukua dakika 12 na sekunde 26, alisema kuwa anashanga kwa nini wataalamu hao wa ujenzi hawajamwandalia sherehe ya kumwaga kama walivyofanya kwa Rais, lakini akasema anaamini wana matumaini fulani, hivyo watakuwa wanajiandaa kumfanyia sherehe ya kumpokea mara baada ya kuingia Ikulu mwishoni mwa mwaka huu akiwaomba wasimsahau katika ‘ufalme wao’.


“Kama ndiyo hivyo basi Mungu awabariki, tuliombee taifa tupite salama katika uchaguzi” alisema Dk Magufuli.


Dk Magufuli naye alimtupia kijembe mmoja wa wagombea urais kupitia vyama vya upinzani aliyesema kuwa akiingia Ikulu anawasaidia waendesha bodaboda akisema mtu huyo kasahau kujiuliza vyombo hivyo vya usafiri vililetwa na nani.

Na Goodluck Eliona na Expuerius Kachenje-Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post