KIMBUNGA CHA LOWASSA CHALETA BALAA- MGOMBEA UBUNGE WA CCM AHAMIA CHADEMA SHINYANGA




Mgombea ubunge jimbo la Shinyanga mjini Charles Shigino kupitia CCM akizungumza na wakazi wa Shinyanga mjini Julai 29,2015 kunadi sera zake ili apewe ridhaa ya kugombea ubunge kupitia CCM kati ya wanachama 10 wa chama hicho waliojitokeza kuwania nafasi hiyo-Picha na Kadama Malunde- Malunde1 blog Shinyanga

Ndugu Charles Shigino akizungumza na waaandishi wa habari mkoa wa Shinyanga wakati akitangaza kukatiza safari yake ya Ubunge kupitia CCM na kuhamia CHADEMA leo Julai 30,2015-Picha na Kadama Malunde- Malunde1 blog Shinyanga

******** 
Kutokana na kile wataalam wa mambo ya siasa wanasema ni kimbunga cha mheshimiwa Edward Lowassa,,katika hali isiyokuwa ya kawaida,katibu wa siasa na uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Shinyanga mjini, Charles Shigino aliyekuwa miongoni mwa wagombea 10 wa ubunge katika jimbo la Shinyanga mjini kutangaza rasmi kukihama chama chake cha CCM na kujiunga na CHADEMA.

Shigino ametangaza uamuzi wake huo Leo mbele ya waandishi wa habari mjini Shinyanga na kueleza kuwa moja ya sababu iliyosababisha achukue uamuzi huo ni kuchoshwa na mizengwe iliyomo ndani ya chama hicho inayoenda sanjari na kukiuka taratibu za chama .

Amesema ndani ya Chama cha Mapinduzi mambo mengi yamekuwa hayaendeshwi kwa mujibu wa katiba na taratibu za chama na badala yake kufuata matakwa ya watu binafsi ikiwemo kukithiri kwa vitendo vya rushwa hali inayokidhalilisha chama hicho hivyo hawezi kuendelea na chama hicho.


“Ndugu zangu mimi ni miongoni mwa wana CCM 10 tulioomba kugombea nafasi ya ubunge , lakini mizengwe kumekuwa na mizengwe ya hapa na pale ndani ya chama inayosababishwa na baadhi ya viongozi wa CCM,hii ni hatari sana,alichofanyiwa Lowassa ndiyo nimefanyiwa mimi, nimeona hata kama nikishinda kwenye kura za maoni kuna mipango inafanywa ya jina langu kukatwa kutokana na chuki binafsi”,amesema Shigino.


“Matendo aliyofanyiwa mheshimiwa Edward Lowassa hayana utofauti na mambo niliyofanyiwa na CCM,hata kwenye kampeni za kutaka ridhaa ya kuwa mbunge,kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa maadili kiasi kwamba rushwa inaonekana kitu cha kawaida huku viongozi wakishuhudia vitendo vya ukiukwaji huo wa maadili”,aliongeza Shigino.

Amesema CCM imeshindwa kusimamia maadili kwani viongozi wake wamekuwa hawachukui hatua yoyote kwa wanachama wanaokiuka taratibu za chama hadi kufikia baadhi ya wagombea kuandaa vikundi vya kuzomea wagombea wengine kwenye mikutano.


“Jambo jingine ni kwamba pamoja na kuwa kiongozi wa kiwilaya lakini nimekuwa sishirikishwi kwenye vikao vingi vya kikatiba, mara nyingi ninapotetea haki za wananchi,naambiwa eti mimi ni msaliti, sasa nimechoka na nimeamua kuachana na CCM,na sasa natangaza rasmi kujiunga na CHADEMA na tayari nimechukua fomu kuwania udiwani katika kata ya Ngokolo mjini Shinyanga,” amesema Shigino.


Shigino ameeleza kuwa ameamua kujiunga na Chadema baada ya kuona chama hicho ndicho kinafaa kuwa mkombozi kwa watanzania, ambacho kinasimamia sera zake ipasavyo na kupigania maslahi ya wananchi.

“Natangaza rasmi leo mimi siyo mwanachama tena wa CCM, na nina ambatana na waziri mkuu mstaafu Edward Lowassa kwa umauzi aliouchukua nimemuunga mkono kwa asilimia zote na ndiyo maana nimeamua kumfuata ili tulikomboe taifa hili ambalo linateketea mikononi mwa CCM”, amesema Shigino.

Kaimu katibu wa CHADEMA wilaya ya Shinyanga Mjini, George Kitalama amethibitisha kupokelewa rasmi kwa mwenezi huyo wa CCM na kwamba alikabidhiwa kadi ya CHADEMA juzi pamoja na aliyekuwa diwani wa viti maalum (CCM) kata Ibadakuli Zimila Kalwani.

Kitalama amesema ndani ya kipindi cha wiki moja CHADEMA imepokea zaidi ya wanachama 400 kutoka CCM waliojiunga na chama hicho na kwamba hali hiyo inatokana na wana CCM hao kuchoshwa na mfumo mbovu uliomo ndani ya chama hicho.

Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Shinyanga mjini, Kanali mstaafu Tajiri Maulid alisema hakuwa na taarifa juu ya mwenezi wake kuhamia CHADEMA na kwamba ofisi yake pia haijapata taarifa rasmi juu ya tukio hilo huku akiongeza kuwa Shigino alikuwa mzigo katika chama.

Uamuzi wa Shigino kujiunga Chadema na kuachana na CCM unakuja siku moja tu baada ya kushiriki mkutano wa CCM uliokuwa unafanyika mjini Shinyanga ambapo alieleza kutoridhishwa na mwenendo mzima wa kutafuta wagombea wa chama hicho watakaopeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao.

Akizungumza jana Julai 29,2015,Shigino alieleza kutoridhishwa na kitendo cha baadhi ya wagombea kuwa na makundi ya watu ambao wamekuwa wakidiriki kuzomea baadhi ya wagombea kwenye mikutano ya hadhara huku akisisitiza kuwa vitendo vya rushwa vimekithiri katika chama hicho.

Na Kadama Malunde- Malunde1 blog Shinyanga

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527