NG'OMBE 800 WAKAMATWA HUKO SIRARI WAKISAFIRISHWA KWENDA KENYA

Ng’ombe zaidi ya 800 waliokuwa wakisafirishwa kwenda nchi jirani ya Kenya kupitia mpaka wa Sirari wamekamatwa na mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Tarime baada ya wafanyabiashara watano kugoma kulipa ushuru wa shilingi elfu tano kwa kila Ng’ombe mmoja.

Wafanyabiashara hao waligoma kutoa ushuru huo kwa madai kuwa ni kinyume na waraka wa katibu mkuu wa wizara ya maendeleo ya mifugo na uvuvi unaowataka wafanyabiashara wenye vibali vya kusafirisha mifugo nje ya nchi kutobughudhiwa mahali popote.


Waraka huo wa Aprili 9 mwaka 2014 unaeleza kuwa mfanyabiashara wa mifugo mwenye leseni ya kitaifa inayomruhusu kununua na kusafirisha mifugo kwenda nchi ya jirani anapaswa kulipa ushuru wa shilingi 20,000 kwa kila Ng’ombe, huku Mbuzi na Kondoo wakitakiwa kulipiwa shilingi 5,000 na baada ya malipo hayo mfanyabiashara wa mifugo hapaswi tena kulipa ushuru au kuchangia huduma nyingine.
 
Wakizungumza katika eneo la mpaka wa Sirari wilayani Tarime baadhi wafanyabiashara hao wamelalamikia hali hiyo na kudai kuwa inaweza kusababisha baadhi ya watu wasio waaminifu kuanza kutumia njia za panya katika kuvusha mifugo yao nje ya nchi kwa lengo la kuepuka usumbufu wa kutozwa ushuru mara mbili.


 
Kwa upande wake mkaguzi wa mifugo wa wizara ya maendeleo ya mifugo na uvuvi Bonaventura Tesha ameeleza kanuni za udhibiti wa usafirishaji wa mifugo zinavyotakiwa kutekelezwa na wafanyabiashara wanaosafirisha mifugo nje ya nchi.


 
Akijibu malalamiko ya wafanyabiashara hao wanaopinga kutozwa ushuru mara mbili, mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Tarime Amos Sagara amesema kazi ya mawakala walioteuliwa na halmashauri hiyo ni kuhakikisha ushuru wa Ng’ombe unalipwa kabla ya mfanyabiashara kusafirisha mifugo nje ya nchi na aina yoyote ile ya ukwepaji haitavulimiwa.

Via>>ITV

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post