Makubwa Haya!! BIBI HARUSI ATOROKA SIKU 4 KABLA YA NDOA,KILICHOFUATIA NI STORI....

MTU mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Juma Mwinyivue maarufu kama ‘Tabambwa’ (28) mkazi wa Zogowale, Visiga mkoani Pwani, alijikuta katika wakati mgumu baada ya mwanamke aliyetarajia kumuoa, aliyetajwa kwa jina moja la Manka (20) kumzimia simu na kuingia mitini siku chache kabla ya ndoa yao, tukio lililotokea Mei 23, mwaka huu.

Juma Mwinyivue maarufu kama ‘Tabambwa' anayedaiwa kutorokwa na mchumbaake.

Kwa mujibu wa mpambe wa bwana harusi, Saidi Matakope, ndugu na marafiki wa bibi harusi walitayarisha ngoma maarufu ya Kigodoro na vyakula wakiamini binti yao atapata mume, lakini hadi ilipofika jioni, mwanaume hakuweza kutokea na kuwaacha watu vinywa wazi.

Katika eneo la tukio, mume mtarajiwa Juma, alisema alikutana na Manka na kumchumbia mwanzoni mwa Machi. 

Baada ya kuridhika na kukubaliana, ndoa ilipangwa kufanyika Mei 23, mwaka huu huku akiwa tayari ameshalipa mahari na kila kitu cha muhimu.

Lakini wiki mbili kabla ya ndoa, Juma alidai kutompata mke wake hewani baada ya kukubaliana kwenda kurekebisha shela la harusi, kitu kilichomshangaza kwani hata alipofika nyumbani kwake, alikuta mlango wa nyumba yake ukiwa umefungwa.

Juma alisema kuwa alipompigia simu yake ilikuwa haipatikani na kuamua kwenda kwa mama yake mzazi ambaye naye hakuwa akijua mwanaye ameelekea wapi huku siku zikiwa ukingoni.
 
Manka anayedaiwa kukimbia ndoa.
“Siku iliyofuata nikampigia mama yake akaniambia mwanaye ameelekea Iringa kwa shangazi yake. Nikashangaa na kuuliza kwa nini hakuniaga. Nilimpigia simu yake ikawa inaita, inakata au kutopatikana kabisa. Kwa hivyo nikamwambia mama mkwe kwamba mwanaye sitamuoa tena na nimesamehe gharama zote nilizotoa,” alisema Juma.

Mshenga wa Juma aliyejitambulisha kwa jina la Kindala, alidai baada ya kumtaarifu mama Manka kuwa ndoa hakuna, alishangaa baada ya wiki moja kupigiwa simu na ndugu zake aliulizwa muda ambao mwanaume angeenda kuoa.

“Ndipo tukashangaa na kuwaambia mbona tayari tumeshatoa taarifa kwa mama mtu kwamba hatuoi tena,” alisema mshenga huyo.

Kwa upande wake, bibi harusi alikiri kusafiri Iringa na shangazi yake, kwa kile alichodai ni kufanyiwa tambiko la ndoa, lakini akaogopa kumuaga mwenzake akijua wazi asingekubaliwa. “Bado nampenda na naitaka ndoa hata kesho nipo tayari, nilikwenda kwa shangazi Iringa siyo kwenye michepuko,” alisema Manka.

Na  Deogratius mongela-GPL

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527