INATISHA SANA!! HEBU ANGALIA PICHA 20 ZA MAFURIKO YALIYOTIKISA DAR ,UNAAMBIWA MVUA ITANYESHA HADI MEI 20,2015!!


 
 
WAKATI mgomo wa mabasi ukimalizika juzi, wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wamekumbwa na adha nyingine, baada ya mvua kubwa zinazoendelea kunyesha kuleta madhara mbalimbali kijamii na kiuchumi.

Katika maeneo mbalimbali ambayo waandishi wetu walitembelea leo, walikuta baadhi ya wakazi wakitoa maji yaliyoingia ndani ya nyumba zao na sehemu za kufanyia bishara zao.
Baadhi ya wakazi wa maeneo ya Mwanayamala Mkwajuni maarufu kama ‘Bondeni’ wameonekana kutupia lawama Kampuni ya ujenzi ya Strabag kuwa ujenzi wao wa barabara ndio umechangia nyumba zao kuingiliwa na maji kwani mifereji iliyotengenezwa haikidhi uwezo wa kusafirisha maji kwa kasi maana ni midogo, badala yake maji hujaa na kupitisha juu kuelekea katika makazi yao.

Wakati huo huo waandishi wetu walifika maeneo ya Jangwani na kukuta baadhi ya nyumba zilizoko bondeni zikiwa zimezama majini, huku wakilalamika kutaka serikali iwasaidie, licha ya ukweli kwamba walishaambiwa siku nyingi kuhama mabondeni.

Wakati huo huo, eneo la soko la Sinza-Afrika Sana, waandishi wetu waliwakuta wafanyabiashara ndogondogo wakilaumu mifereji inayopitisha maji barabarani kuziba kufuatia uchafu unaotupwa na kuziba maji kufika hadi sokoni hali inayopelekea biashara zao kudoda kutokana na wateja kukosa sehemu ya kupita.
Mvua hiyo iliyofikia kipimo cha milimita 132.5 kwa mujibu wa vipimo vilivyofanywa katika kituo cha Shule ya Msingi ya Maktaba, ilisababisha barabara kujaa maji na nyingine kuharibika na madaraja kadhaa kukatika.
 
Mkurugenzi Mkuu wa Hali ya Hewa, Dk Agnes Kijazi alisema jana kwamba kipimo hicho cha mvua ni cha juu mno kulinganisha na kile cha wastani ambacho ni kati ya milimita 16 na 30.
 
“Kwa takwimu za mwezi Mei, kiwango hiki hakijawahi kufikiwa kwa miaka 10 iliyopita.” Alipotakiwa kufafanua miezi mingine, Dk Kijazi alisema hakuwa na takwimu kwa kuwa alikuwa nje ya ofisi.
 
Awali, Dk Kijazi alitoa taarifa ikisema mifumo ya hali ya hewa inaonyesha kuwa “hali ya mvua inatarajiwa kuendelea katika baadhi ya siku hadi Mei 20, mwaka huu”.
 
“Mamlaka inaendelea kushauri wakazi wa maeneo hatarishi pamoja na watumiaji wa bahari kuchukua tahadhari,” alisema Dk Kijazi.
 
Watano wafa
Kutokana na mafuriko hayo, watu watano wakiwamo watoto wawili, walipoteza maisha baada ya kusombwa na maji.
 
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick alisema waliopoteza maisha ni watoto wawili na mzee mmoja ambao majina yao hayajafahamika.
 
“Mtoto mmoja (2) alisombwa na mafuriko katika eneo Machimbo ya Makangarawe na mzee mmoja alifariki jana baada ya mvua kunyesha na kujaa ndani ya nyumba yake. Mtoto mwingine ambaye bado hajapatikana alisombwa na mafuriko pia,” alisema Sadick.
 
Hata hivyo, habari zilizopatikana baadaye zilisema kuwa waliopoteza maisha ni watu watano.
 
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alimtaja mtu aliyefariki dunia kuwa ni Shabani Idd (73) mkazi wa Manzese.
Katika eneo la Mbezi Luis, Mto Mbezi ulifurika, hali iliyosababisha nyumba zilizojengwa kandokando ya daraja hilo kufunikwa na maji.
 
Mkazi wa eneo hilo, John David alisema hali ilikuwa mbaya zaidi jana asubuhi kwani maji yalifurika na kujaa barabarani na kusababisha usumbufu mkubwa kwa watumiaji.
 
Alisema wakazi walio karibu na mto huo walichukua tahadhari tangu juzi na kuhama makazi yao.
 
“Haikuwa rahisi kwa wao kuendelea kukaa hapa wakati wanafahamu hali kama hii ingetokea. Tangu jana jioni familia zinazoishi huko ziliondoka, lakini vitu vyao vimesombwa na maji na nyumba moja imesombwa pia,” alisema David.
 TAZAMA PICHA HAPA CHINI UONE HALI INAVYOTISHA
 







 


Daraja la Kivule lilivyoathiriwa na mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dar.Magari yakipita eneo hilo la daraja kwa tabu.Mkondo wa maji yanayopita darajani hapo.
Hivi ndivyo hali ilivyo katika barabara ya Morogoro eneo la Jangwani.
Baadhi ya nyumba zilizo bondeni katika eneo la Mkwajuni, Kinondoni jijini Dar.
Namna ambavyo soko la Sinza-Afrika Sana linavyoonekana kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dar.
Mkazi wa Tandale kwa Tumbo akitoa maji yaliyojaa kwenye nyumba yake kufuatia mvua kali zinazoendelea kunyesha jijini Dar.
Wakazi wa Tandale kwa Tumbo na maeneo ya jirani wakipita kwa tabu katika njia hiyo kufuatia mvua ambazo zinaendelea kunyesha jijini Dar.
 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post