Hali Mbaya!! WAGONJWA WA UGONJWA WA AJABU HUKO SIMIYU WAFIKIA 1000!!

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu elaston Mbwilo akiongea na wananchi katika wilaya ya Meatu.

Idadi ya wagonja ambao wameugua ugunjwa wa ajabu uliozikumba jumla ya kata 6 katika wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu imezidi kuongezeka kila mara, tangu kuripotiwa kutokea kwa ugonjwa huo wiki mbili zilizopita.

Mpaka jana taarifa zilizotolewa na Mganga Mkuu wa wilaya ya Meatu Adamu Jimisha alisema kuwa idadi hiyo imeongezeka kutoka wagonjwa 80 hadi kufikia 1048 ambao walifikishwa katika kituo cha afya Mwandoya.

Jimishi alitoa taarifa hiyo mbele ya kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa, iliyokuwa ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa Erasto Mbwilo, alipowatembelea baadhi ya wagonjwa waliokuwa wamelazwa katika kituo hicho cha afya pamoja na kata za, Mwabusalu, Lingeka, Mwakisandu, Tindabuligi, Pamoja na Lubiga ambazo zimekubwa na janga hilo.

Alieleza kuwa bado dalili za baadhi ya wagonjwa ambao wamekuwa waliletwa katika kituo hicho cha afya tangu kutokea kwake, zimekuwa ni zile zile kuumwa kichwa, kikohozi kikavu, mwili kulegea, kuchanganyikiwa akili pamoja na kupoteza fahamu.

Aliongeza kuwa wagonjwa hao wamekuwa wakitibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani pindi wanapopata nafuu au kupona kabisa, huku akibainisha kuwa baadhi yao walikutwa na magonjwa mbalimbali kama malaria na minyoo.

Mganga Mkuu huyo alieleza kuwa wataalam wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii wakiambatana na Timu ya Mkoa akiwemo Mganga Mkuu wa Mkoa, Mtaalam wa Maabara na Daktari mmoja walichukua sampuli kwa ajili ya kupeleka Nairobi kwa Uchunguzi.

Alisema timu hiyo ilipeleka vipimo hivyo tarehe 15/05/2015 kwa ajili ya kubaini aina gani ya ugonjwa, ambapo majibu alieleza kuwa timu hiyo iliahidi kutoa mwishoni mwa mwezi huu.

Kwa upande wake mkuu wa Mkoa aliwataka wananchi wa Wilaya hiyo waliokuwa wamefika kuwajulia hali baadhi ya wagonjwa katika kutoa hicho cha afya kuwapeleka mapema hospitali watu watakaoonekana kuwa na dalili za ugonjwa huo.


“ Msiiwaache wagonjwa majumbani waleteni na msiwapeleke kwa waganga wa kienyeji,  mkiona watu wenye dalili za ugonjwa kama walivyowaeleza wataalam waleteni haraka hapa Mwandoya wapatiwe matibabu” ,alisema Mbwilo.

Mbwilo aliwaeleza wananchi kuwa kwa mujibu wa Watalaam wa Afya  ugonjwa huo hauna madhara ya kifo, hivyo akawataka kuendelea na shughuli zao kama kawaida wakati Serikali inaendelea kufanya uchunguzi juu ya chanzo cha ugonjwa huo.

Nao baadhi ya wananchi wakiongea mbele ya mkuu huyo wa Mkoa waliiomba Serikali kufuatilia haraka matokeo ya vipimo vilivyochukuliwa na Wataalam hao ili wajue chanzo cha ugonjwa huo ambao mpaka sasa hawaujajulikana.

 “Tunaomba majibu ya vipimo vilivyochukuliwa yaletwe haraka, maana mpaka sasa hivi hatujui huu ni ugonjwa gani na chanzo chake nini, Serikali itusaidie katika hili” alisema mmoja wa wananchi alijulikana kwa jina la Joseph.


Mhe Mbwilo alisema Serikali inaendelea kufuatilia majibu ya vipimo hivyo vilivyochukuliwa na Timu ya Wataalam wa Afya  kutoka Mkoa wa Simiyu na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii  baada ya kukamilisha taarifa zitatolewa kwa wananchi.

Via>>Simiyunews blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post