WAHAMIAJI 7 WAKAMATWA SHINYANGA WAKIENDA AFRIKA KUSINI,WAMO KUTOKA SOMALIA NA ETHIOPIA!!


Wahamiaji haramu saba kutoka nchi ya Somalia na Ethiopia wamekamatwa mkoani Shinyanga wakiwa kwenye magari ya abiria kuelekea jijini Dar es salaam na wilayani Kahama na baadaye kusafirishwa kwenda nchini Afrika Kusini.

Kamanda  wa polisi mkoa wa Shinyanga Justus Kamugisha amesema wahamiaji hao haramu wamekamatwa Aprili 26 na 27 mwaka huu katika nyakati mbili tofauti kufuatia msako na doria ya askari wa jeshi la polisi.

 Miongoni mwa  waliowakamatwa wamo  raia wanne wa Somalia ambao walikamatwa katika kijiji cha Isela kata ya Samuye wilaya ya Shinyanga Vijijini wakiwa kwenye basi dogo lenye namba za usajili T.866 DCQ fuso inayojulikana kwa jina la Tiger Bus.

Amewataja wahamiaji hao kuwa  Dasent Taraky(15),Abuu Undure(30) Tagasa Aebete(25) na Izrael Abunne(18) ambao walikuwa wakisafiri kutoka Mwanza kuelekea Kahama .

Amesema raia hao wa kigeni walikuwa wakisafirishwa na Issa Juma(21) na Maulid Juma (19) wote wa kazi wa Majengo wilayani Kahama ambao pia wanashikiliwa na jeshi la polisi.

Amesema kundi la pili la wahamiaji waliokamatwa ni la raia watatu kutoka nchi ya Ethiopia ambao walikamatwa Aprili katika stendi ya mabasi ya Ibinzamata mjini Shinyanga wakitokea mkoani Mwanza kuelekea jijini Dar es salaam katika basi lenye namba za usajili T.974 YOUTONG mali ya kampuni ya Master City na walikuwa wanasafirishwa na watu ambao hawajafahamika.

Kamanda Kamugisha amewataja wahamiaji hao kuwa ni Fireza Wehmebo(19),Dawiti Esatu(18) na Dagafa Geje(18) wote wakazi wa South Hawasa nchini Ethiopia.

Kamanda Kamugisha amewataka watanzania kuacha tabia ya kujihusisha na vitendo vya kuwahifadhi na kuwasafirisha watu hao na atakayekamatwa atafikishwa mahakamani na sheria itachukua mkondo wake.

Kwa upande wao watanzania wanaotuhumiwa kuwasafirisha wahamiaji hao haramu  wamesema wao wametumwa kuwachukua watu hao mkoani Mwanza na kuwafikisha katika mji wa Kahama ambapo mtu mwingine atawachukua na kuwapeleka Afrika Kusini kupitia Dar es salaam huku wahamiaji hao haramu wakidai kuwa wanasafiri kwenda Afrika Kusini kutafuta maisha mazuri kwa kua nchini kwao hali ya maisha ni duni.

Na Kadama Malunde-Shinyanga

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527