Mwanamke
mmoja, mkazi wa Mabibo Mwisho, jijini Dar es Salaam, anadaiwa kuanzisha
danguro la wasichana na kuendesha biashara ya ngono ikiwamo ya jinsia
moja.
Mwanamke huyo anayefahamika kwa jina la mama Uzuri, anadaiwa kuwachukua
wasichana hao kutoka vijijini kwa kuwadanganya kuwa anakwenda
kuwatafutia kazi mjini.
Inadaiwa kuwa fedha anazopata kutokana na biashara hiyo, huzitumia kama gharama ya kuwatunza wasichana hao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wasichana hao
(majina yanahifadhiwa), walidai kuwa mwanamke huyo aliwachukua vijijini
kwao kwa ahadi ya ajira za ndani.
Wakielezea undani wa biashara hiyo, walisema wanaume wengi wamekuwa
wakiwalazimisha kufanya mapenzi bila kinga (kondom), kwa madai kuwa kwa
kufanya hivyo kunawanyima starehe ya tendo hilo.
Suzana (sio jina lake halisi), alisema makazi yao ni nyumbani kwa
mwanamke huyo ambapo hulelewa katika mazingira mazuri, na kati yao kuna
makahaba na wasagaji.
Alisema, mwanzo walipoanza biashara hiyo walipata wakati mgumu lakini kadiri siku zinavyokwenda waliizoea.
Alisema baadhi yao wanachukuliwa na wanaume zaidi ya mmoja kwa siku na
wakati mwingine hugeuka kuwa walimu kwa wasichana wapya wanaoletwa
kutoka vijijini.
“Wakati nachukuliwa kwa wazazi wangu, mwajiri wangu aliwaeleza kwamba
nakuja kufanya kazi za ndani kwa ndugu yake, na kamwe sitopata madhara
yoyote kutokana na ulinzi na usimamizi nitakaoandaliwa, lakini baada ya
kufika hali ikawa tofauti," alisema na kuongeza:
“Nilipokelewa vizuri na wasichana wenzangu niliowakuta, lakini
nilishangazwa na kauli ya mwajiri wangu kuwa nahitaji kufanyiwa
ukarabati wa kutosha, na akatoa agizo kutofanyishwa kazi yoyote badala
yake nipumzike na nitaandaliwa kila kitu ninachokitaka, lakini
atakaponituma sehemu na wenzangu nikatekeleze kama atakavyoniagiza,
alisema Suzana.
Uchunguzi wa NIPASHE katika mahojiano na mwanamke huyo, alisema ni
vigumu kuiacha biashara hiyo kwa sababu aliianzisha siku nyingi akiwa na
wasichana watano.
Alisema wasichana hao amewaajiri kwa gharama kutokana na shughuli
wanazozifanya, na wanapokwenda kijijini kwa wazazi wao, huwagharamia
matumizi na zawadi kwa familia zao.
Alisema gharama za biashara hiyo hutofautiana kulingana na kiwango cha
mteja, lakini kwa wale wanaofanyiwa tendo hilo kinyume na maumbile,
wateja hutozwa Sh. 20,000, na ngono ya kawaida Sh. 5,000 hadi Sh.10,000
kwa mara moja.
Aidha, alisema wanaofanya tendo hilo kwa jinsia moja (wasagaji), gharama zake hazitofautiani.
“Kifupi wasichana wangu wanajituma hata wateja wenyewe wanawakubali
ndani na nje ya Dar es Salaam, lakini biashara ina msimu, kuna wakati
inakulipa na wakati mwingine inasuasua.
“Kikubwa ni ujanja na namna ya kuwaandaa wasichana, kwa bahati nzuri
katika familia zao hakuna anayejua kazi anayoifanya mtoto wake zaidi ya
‘house girl’. Ni marufuku kutoa siri ya kazi hivyo ni lazima niwekeze
kwao kwa gharama yoyote maana najua wanachokifanya mjini,” alijitapa
mwanamke huyo.
Alisema ingawa anajua kuna maradhi lakini amekuwa mstari wa mbele kutoa
elimu kwao ili waweze kujikinga na magonjwa hatari yanayoenezwa kwa njia
ya ngono pamoja na ugonjwa hatari wa Ukimwi.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
Social Plugin