ANGALIA PICHA JINSI PROFESA LIPUMBA ALIVYOSHIKWA TANGANYIKA JESHI NA ASKARI KANZU KISHA KUPANDISHWA KWENYE GARI LA POLISI






ANGALIA PICHA HAPA CHINI MWONEKANO WA PROF. LIPUMBA,DAKIKA CHACHE TU BAADA YA KUACHIWA

Hapa anakumbatiana na Katibu Mkuu wa NCCR.Jeshi la Polisi jana ilitumia nguvu kuwatawanya wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF), kwa kurusha mabomu, risasi za moto na maji ya kuwasha, na kumkamata Mwenyekiti wa chama hicho, Prof. Ibrahim Lipumba na wafuasi wengine wapatao 32.
Nguvu hiyo ya Polisi ilitumika wakati wa kuzuia msafara wa Mwenyekiti huyo kuelekea eneo la Zakhem, Mbagala, kulikokuwa kumeandaliwa na mkutano wa hadhara, kutoa taarifa kwa wafuasi waliokuwa wamekusanyika, kuwa mkutano na maandamano yamezuiliwa na Polisi.
Mkutano huo ambao ungetanguliwa na maadamano kutoka ofisi za wilaya ya Temeke kwenda Zakhem kwa ajili ya kumbukumbu ya miaka 14 ya mauaji ya wafuasi wake zaidi ya 30 waliouawa Januari 27, 2001 na Jeshi la Polisi Zanzibar wakati wa maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais wa Zanzibar wa mwaka 2000.
Kutokana na purukushani hizo za jana, polisi wenye silaha na virungu walitembeza kichapo kikali kwa wafuasi waliokahidi amri ya polisi kuwa taka watawanyike, huku wakiwashusha waliokuwa kwenye magari.
Baada ya kipigo cha dakika 30, polisi wakiongozwa na S .Zacharia, ambaye mara kwa mara alizungumza na Prof. Lipumba na viongozi wengine kutawanyika bila mafanikio, walimteremsha kwenye gari na kumpakiza kwenye gari ya polisi.
Katika kamatakamata hiyo wafuasi zaidi ya 15 walitembezewa kichapo na kuswekwa kwenye gari tatu za polisi, huku katika gari lililombeba Prof. Lipumba akiwa na wafuasi wengine wawili.
Kabla ya purukushani hizo, Mwenyekiti wa Lipumba akiwa kwenye msafara wa magari matatu waliotoka katika ofisi za Makao Makuu yaliyoko Bunguruni hadi ofisi ya Wilaya ya Temeke na kuzungumza na wanachama waliofurika kwenye ofisi hizo tayari kwa maandamano waliyokuwa wametangaziwa.
Baada ya kuwasili katika ofisi hizo, aliwaeleza wafuasi wake kuwa maandamano yaliyokuwa yamepangwa kufanyika kutokea ofisini humo ( Temeke) hadi Zakhem Mbagala, yamezuiwa na polisi, hivyo ni vema yasifanyike na kwamba atakwenda kutoa taarifa kwa wananchi waliokuwa nyoka eneo la Zakhem.
Baada ya kutoa taarifa hizo, wafuasi hao walionekana kutoridhika na kuanza kupiga kelele huku wakidai wako tayari kufa, lakini waandamane.
Mwenyekiti huyo alipata wakati mgumu  kuwatuliza wafuasi hao ambao walipinga kauli ya kutoandamana na kudai hata kama kiongozi huyo atakwenda kwa gari watatembea kwa miguu au kupanda daladala kumfuta kwenye mkutano.
Alisema katika barua ya polisi iliyopelekwa ofisi za CUF, Januari 26, mwaka huu, saa 12:30 jioni, ilitoa sababu tatu za kuzuia maandamano hayo.
Prof. Lipumba alisoma barua hiyo kuwa ilieeleza Kaimu Kamishna wa Kanda Maalum wa Polisi, akieleza baada ya kutafakari kwa kina wamezuia maandamano hayo kwa madai kuwa siyo halali.
Alinukuu barua hiyo kuwa maandamano ya Januari 27, mwaka 2001, hayakuwa halali, hivyo maandamano ya kumbukumbu ya mauaji ya wafuasi wa chama hicho Zanzibar nayo siyo halali na hivyo hawatakiwi kuyafanya.
Aliendelea kumnukuu kuwa sababu nyingine zilizotolewa na polisi ni kuwa taarifa za kiitelejensia zinaonyesha kuwa kutakuwa na vurugu, kuvunjika kwa amani na watu kujeruhiwa, hivyo hakuna sababu za wafuasi hao kuandamana wala kufanya mkutano.
Prof. Lipumba alisema sababu nyingine waliyotoa ni tishio la vitendo vya kigaidi, hivyo maisha ya waandamanaji yatakuwa hatarini kwa kuwa kuna uwezekano wa tukio la kigaidi kutokea.
Muda wote ambao kiongozi huyo akiongea na wafuasi hao, Polisi wakiwa kwenye magari walionekana wakipiga doria za hapa na pale, hali iliyowafanya wafuasi hao mara kwa mara kufuatilia kilichokuwa kikiendelea.
Akizungumza baada ya kusoma barua hiyo, alisema Polisi inaona ni halali watu kufa, lakini ni haramu kufanya maandamano kwa ajili ya kumbukumbu ya kifo cha watu hao.
“Leo tungewaandikia barua kuwa tunaandamana kuunga mkono ufisadi na wizi ndani ya serikali wangetuunga mkono, na Chama Cha Mapinduzi kikitaka kuandamana kingepewa na mara kwa mara wanaandamana bila kubugudhiwa," alisema.
Mwenyekiti huyo alisema vyama vya siasa vinatumia sheria namba tano ya vyama vya siasa kuomba kibali cha polisi kufanya mkutano wa hadhara na maandamano, lakini polisi wanatumia sheria namba 43 sura ya 322, kuzuia maandamano na mikutano ya vyama vya upinzania kwa sababu zao.
Alisema Tanzania inakabiliwa na matatizo mengi kubwa ikiwa ni kukosekana kwa utawala bora na demokrasia na kwamba maandamano ya Januari 27, mwaka 2001, yalilenga kushinikiza uwepo wa Katiba mpya, utawala bora na demokrasia, lakini wafuasi waliuawa.
"Leo tunawajibu kwa wenzetu 60 ambao waliokufa  wakati wakipigana haki, haki haipatikani katika sinia la ubwabwa bali inapiganiwa, woga ni adui wa haki, tuondoe woga tusonge mbele hii ni nchi yetu sote, polisi wanaona ninaongea nanyi hapa wanapita na magari yao kuwatisha," alisema.
Alisema baada ya kupata barua hiyo na kutafakari malengo makuu ya chama hicho, wameona wasiandamane, lakini kwa kuwa katika eneo la Zakhem kuna wananchi waliokuwa nyoka ni vyema akapenda kuwapa taarifa na wananchi wa eneo hilo (Temeke), waendelee na shughuli nyingine.
Alisema polisi wamefanya makusudi kwa kuwa taarifa za maandamano na mkutano huo walikuwa nazo tangu Januari 22, mwaka huu, lakini kwa makusudi wakijibu barua na kuiwasilisha ofisini muda ambao ofisi zimefungwa na wanachama walishapewa taarifa.
Baada ya kumaliza kuzungumza na wafuasi hao, Mwenyekiti huyo na wafuasi wengine walioingia kwenye magari, na baada ya kutembea mita chache kando na hospitali ya wilaya ya Temeke, walikuta polisi wenye magari madogo na gari kubwa la maji ya kuwasha wakiwa wamefunga barabara.
Baada ya hali hiyo kiongozi huyo na wafuasi wengine waliteremka na afande S. Zacharia ambaye alijitambulisha kama Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Temeke, alisema hawana taarifa za maandamano wala mkutano, hivyo wanamtaka arudi alikotoka.
Prof. Lipumba aliwaeleza kuwa wana barua iliyowakataza kufanya maandamano na mkutano, lakini kwa kuwa eneo la Zakhem kuna wafuasi waliokusanyika anakwenda kuwapa taarifa, jambo ambalo lilipingwa vikali na polisi waliokuwapo.
Hata hivyo, jitihada za viongozi wa CUF kuzungumza na viongozi hao wa polisi zilishindikana kutokana na viongozi wa Polisi kudai kuwa hawana taarifa na kumtaka Mwenyekiti huyo kutopelekwa eneo la Zakhem.
Baada ya mabishano ya dakika 20, msafara wa Prof. Lipumba uliendelea na walipofika kwenye mzunguko wa Mtongani, magari ya polisi yalifunga barabara.
Lipumba na wenzake  waliteremka na kuongea na polisi hao bila mafanikio na baadaye alionekana kachero mmoja wa polisi akiwa amevalia kiraia, akiwataka kutawanyika na kuwaeleza kuwa hawaruhusiwi kuendelea na safari.
Baada ya kauli hiyo, alijitokeza ofisa wa polisi ambaye alitangaza tahadhari ya kutaka watu kutawanyika na askari kuamriwa kuanza kurusha risasi na mabomu hewani huku maji ya kuwasha yakimwagwa.
Purukushani hiyo iliambatana na kichapo kwa wafuasi waliokuwa ndani ya magari manne ya CUF, likiwamo gari la waandishi wa habari na Prof. Lipumba, kufunguliwa milango na waliokuwa ndani kuanza kushushiwa kipigo kikali.
Polisi walionekana wakiwashambulia wafuasi hao kwa dakika 30 na kuwasweka kwenye magari ya polisi na kuondoka nao, akiwamo Prof. Lipumba.
Wananchi waliokuwa eneo hilo walitawanyika huku wengine wakifunga biashara zao na kukimbia ovyo, ikiwa ni pamoja na kutafuta maji ya kunawa kutokana na mabomu ya machozi yaliyokuwa yanarushwa.
Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro, alisema wamekamatwa kwa,sababu walifanya maandamano bila kupata kibali cha polisi.
“Waliomba kibali, lakini walinyimwa kwa sababu za kiusalama, wao wametumia nguvu kufanya maandamano yasiyo rasmi,” alisema Sirro.
Alisema watu 32 akiwamo Prof. Lipumba walitiwa mbaroni na kwamba wanaume ni 30 na wanawake wawili na kuongeza kuwa walikuwa wakiendelea kuhojiwa jana jioni katika Kituo Kikuu cha Polisi. 
CHANZO: CHA HABARI NIPASHE

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527