Mwili wa marehemu Daudi
Lusalula Mbatiro(56) baada ya kuchinjwa Desemba 5,2014-Picha kutoka maktaba ya malunde1 blog
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Justus Kamugisha
Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga limefanikiwa kunasa
mtandao wa watu wanaojihusisha na vitendo vya mauaji ya watu kwa kuchinja kwa
visu,ikiwemo tukio la mauaji ya Katibu wa Chama
Chama Mapinduzi kata ya Mwalugulu wilayani Kahama mkoani Shinyanga Daudi
Lusalula Mbatiro(56) aliyeuawa kwa kuchinjwa kama kuku mwaka jana kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa.
Tukio la kuuawa kwa katibu huyo wa CCM lilitokea Desemba 5,2014 saa mbili usiku wakati katibu
huyo wa CCM kata ya Mwaluguru ambaye pia alikuwa ni katibu wa elimu,malezi na mazingira baraza la
wazazi wa CCM wilaya ya Kahama akitokea kata ya Kagongwa kwenda nyumbani
kwake Sungamile baada ya kutoka kwenye mkutano wa chama chake uliokuwa unafanyika mjini Kahama.
Waliotajwa na jeshi la polisi kuhusika katika
mtandao huo ni pamoja na diwani wa kata ya Mwalugulu wilayani Kahama Bundala
Kadilanha(CCM),mfanyabiashara wa Kagongwa Tobo Mwanasana,pamoja na Emmanuel
Maziku,Masanja Shepa,Samwel Seni Budugu na Shija Shepa.
Kwa mujibu wa taarifa ya
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Justus Kamugisha alisema katika uchunguzi
wa mauaji ya katibu wa CCM kata ya Mwalugulu Daudi Mbatiro jeshi la polisi
limewakamata watuhumiwa Emmanuel Maziku na Masanja Shepa na baada ya kuhojiwa
walikiri kuhusika na mauaji hayo.
Alisema baada ya kuwahoji
watuhumiwa hao wawili,waliwataja wahusika wengine ambao ni Bundala
Kadilanha(diwani wa Mwalugulu),Tobo Mwanasana(mfanyabiashara,Samweli Seni
Budugu mkazi wa Mwakitolyo na Shija
Shepa mkazi wa Mwalumba Kahama.
Alisema awali jeshi la polisi
baada ya kupata taarifa za watu hao liliweka mtego kwa kuwapigia simu ili
kuwakodi kufanya mauaji katika kijiji cha Nyindu na kufanikisha kuwakamata watu hao ambao
hujihusisha na matukio mbalimbali ya mauaji.
Alisema baada ya kuwafanyia
mahojiano watu hao wawili walikiri kuhusika na matukio ya mauaji katika mkoa wa
Shinyanga na Tabora kwa kukodiwa ili kuchinja watu kwa kisu na wao sio wakata
mapanga ingawa wanaua vikongwe na kulipiza kisasi.
Kamanda Kamugisha alisema watuhumiwa
walisema kiongozi wao ni Samweli Seni Budugu na wenzake ni Tobo
Mwanasana,Bundala Kadilanha na Shija Shepa na kabla ya mauaji hayo wanaenda
kupakwa dawa kwa waganga wao wa jadi ambao ni John Shija mkazi wa kijiji cha
Lyabukande na mwingine aliyetajwa kwa jina moja la Tabu mkazi wa Kizungu.
Kamanda Kamugisha alisema
watuhumiwa wote wamekiri pia kuhusika na matukio ya mauaji ya marehemu Ngolo
Sakumi(69) mkazi wa Mwalugulu na walikodiwa kwa shilingi 1,000,000/=
aliyewakodi ni Jikuba Kajile na Lukuba Nangi.
Tukio jingine walilokiri
kuhusika ni mauaji ya Mary Seleman Masenya(45) mkazi wa kijiji cha Matinje na
walikodiwa kwa shilingi 800,000/= na wanawake watatu ambao ni wake wenza wa
marehemu.
Alitaja tukio jingine
walilohusika ni lile la mauaji ya Mboje Seni(70) mkazi wa kijiji cha Butondo na
walikodiwa kwa shilingi 800,000/= walikodiwa na Mwanabundi mkazi wa Butondo na
tukio jingine ni mauaji ya Kwigema Lubinza(60) mkazi wa kijiji cha Kakulu kata
ya Nyahanga.
Kamanda huyo alisema jeshi la
polisi linaendelea na msako wa kuwakamata wahusika wengine wa matukio hayo
ikiwa ni pamoja na waganga wa kienyeji waliohusika huku akiwataka wananchi
kutoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa wahusika wote wa mauaji ya kukodiwa
na mauaji ya vikongwe ili kukomesha kabisa mauaji hayo.
Na Kadama Malunde-Shinyanga