Hatari!! WATOTO 198 WANUSURIKA KUAMBUKIZWA VIRUSI VYA UKIMWI SHINYANGA

Mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dkt Ntuli Kapologwe

Jumla ya Watoto 200 waliozaliwa mwaka uliopita(2014), ambao wazazi wao walipimwa na kukutwa na maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU), Mkoani Shinyanga, watoto 198 kati yao ndiyo walionusurika na maambukizi ya ugonjwa huo, baada ya kuzaliwa salama, huku wawili wakibainika kuwa wameathirika.

Mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dkt Ntuli Kapologwe ameyasema hayo wakati akizungumza na Malunde1 blog, kuhusiana na mikakati ya mkoa kupunguza maambukizi mapya ya (VVU),kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Dkta Kapologwe amesema mwaka 2014) jumla ya akina mama wajawazito 200, waliobainika kuwa na maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU),waliofika kliniki na kupimwa katika Zahanati, Vituo vya afya, hospitali za wilaya na mkoa, walianza kupatiwa dawa za kuzuia maambukizi hayo mapya kwenda kwa mtoto, ambapo wazazi 198, walijifungua watoto wasiokuwa na maambukizi ya VVU.

“Baada ya akina mama wajawazito hao kupimwa na kubainika kuwa wana maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU), ndipo wakaanza kupatiwa dawa mara moja, ili kuzuia maambukizi mapya kwenda kwa mtoto, ambapo akina mama tuliwapa dawa inayoitwa TLE,(TEMOFOVIR LAMIVUDINE  EFAVERENZ)”,alifafanua Dkt Kapologwe.

"Watoto pia tuliwapatia dawa inayoitwa Niverapine, ambayo nayo inazuia mtoto asipate maambukizi hayo mapya ya (VVU),kutoka kwa mama",aliongeza Dkt Kapologwe.
 Amesema watoto hao wamenusurika kupata VVU kutokana na akina mama hao kujitokeza kupima afya zao na kufuata masharti na kuongeza kuwa  changamoto kubwa iliyopo katika mkoa wa Shinyanga ni akina mama wengi kutofika kliniki na wengine kukimbilia kwa wakunga wa jadi na kujifungulia majumbani hali ambayo inachangia vifo vingi vya watoto.

"Tunasisitiza akina mama kuhudhuria kliniki ili kujua afya zao,lakini pia kujifungulia hospitali kwani vifo vingi vya watoto na akina mama vinachangiwa na akina mama wajawazito kutofika hospitali kutokana na akina mama hao kuchelewa kupata huduma",alisema Dkt Kapologwe.

"Siku hizi akina mama wengi wanajifungua watoto wakubwa mfano kuanzia kilo 3.5 hadi 5,mtoto anaweza kuzaliwa na kasoro kama hujafika hospitali unaweza kusababisha kifo cha mtoto huyo,kwa hiyo ",aliongeza.

Amesema mwaka 2014 katika mkoa wa Shinyanga jumla ya watoto 98 wenye chini ya umri wa mwezi mmoja walifariki dunia kutokana na sababu mbalimbali.
 
Na Kadama Malunde-Shinyanga





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527