Makubwa Haya!!! KELELE ZA HARUSI ZAUA MTU JIJINI DAR ES SALAAM

 
Mkazi wa Dar es Salaam, Goodluck Madaraka anayedaiwa kujeruhiwa na risasi wakati wa mkesha wa sherehe ya harusi eneo la Tabata Kisukulu usiku wa kuamkia jana, akiwa katika eneo hilo lililogeuka kuwa la msiba jana, baada ya mwenzake Salim Ally kudaiwa kuuawa kwa risasi na jirani yao aliyekerwa na kelele za muziki wakati wa sherehe hiyo. Picha na Kalunde Jamal  


Katika hali isiyokuwa ya kawaida, mwanamume mmoja amewafyatulia risasi watu wawili na kusababisha kifo cha mmoja kwa kile kinachodaiwa kumletea usumbufu wakati wa mkesha wa harusi. 

Mkuu wa Upelelezi  wa Mkoa wa Ilala, David Mnyambuga amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ingawa hakuwa tayari kulizungumzia kwa madai kuwa siyo msemaji na anayetakiwa kufanya hivyo  ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala ambaye hakupatikana kulizungumzia hilo.
Majeruhi wa tukio hilo, Goodluck Madaraka aliyejeruhiwa na risasi zilipokuwa zinapigwa hewani, alisema saa tano na nusu usiku walipokuwa wanacheza muziki kwenye mkesha wa harusi, ghafla jirani yao aliyefahamika kwa jina la Lucas Muhabe alikuja na panga na kuwafukuza kwa madai kuwa wanampigia kelele.
Alisema Muhabe aliondoka na baada ya muda alirudi na bastola na kupiga risasi ovyo na kwa bahati mbaya ikampata begani Mahamudu Muhasi aliyekuwa anapita njia na kumpiga nyingine ya kichwa na kumuua papo hapo.
“Muhasi alikuwa anapita njia hivyo hata vijana walivyokimbia yeye hakukimbia na alipopigwa risasi ya bega la kushoto alilalama kumwambia huyo baba kuwa anamwonea kwani hafahamu kitu chochote, cha kushangaza baada ya kuambiwa hivyo aligeuka na kumpiga nyingine ya kichwa na kufariki dunia papo hapo,” alisema Madaraka.
Madaraka alisema kuwa kwenye heka heka za kupigwa risasi hizo moja ilimpitia kwenye shavu na kumpasua na alikwenda Hospitali ya Amana na kushonwa nyuzi tatu.
Kaka wa marehemu, Salim Ally alisema kuwa Muhasi alikuwa anashinda kwake na kulala kwa mjomba wake mbali kidogo kutoka kwake, siku ya tukio baada ya kula chakula cha usiku na kuzungumza hadi saa tano usiku, alimsindikiza.
Alisema alipohakikisha wamepita kwenye maeneo ambayo hakuamini kama ni salama, alimwacha aende mwenyewe, njia kuu ikiwa ni hapo palipokuwa na mkesha wa harusi na alipata taarifa ndugu yake ameuawa kwa kupigwa risasi.
“Amekuja mwezi wa saba kutoka Malinyi Ulanga, siyo mwenyeji na wala hashindi maeneo hayo, ndiyo maana hata wakati vijana wanakimbia alikuwa anashangaa tu ndiyo akapigwa risasi, inauma sana hata siamini kama sheria itachukua mkondo wake kwa jinsi ninavyoumia,” alisema Ally.
Ally aliongeza kuwa, tunasikia mtuhumiwa amesema marehemu ni jambazi ndiyo maana amempiga risasi, kitu ambacho siyo kweli hana historia hiyo na ni mgeni hapa jijini.
Akizungumza na gazeti hili Mtawala Amani ambaye nyumbani kwake ndiyo kulikuwa na mkesha wa harusi, alisema muda wa saa tatu aliamua kujipumzisha barazani aliamshwa mnamo saa tano na nusu na kelele zilizokuwa zinatokea nje ya nyumba yake.
Alisema baada ya kutoka nje alikuta damu na mwili wa kijana Muhasi na kuambiwa kuwa jirani yao Lucas Muhabi ndiyo amemuua kwa kumpiga risasi na muda siyo mrefu polisi walifika na kuuchukua mwili kuupeleka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

 Mke wa Amani, Pili Miraji alisema kuwa anamfahamu marehemu kwa kuwa alikuwa akimwona anapita maeneo hayo na anakwenda kwa mjomba wake ambako siyo mbali kutoka hapo kwao.

 Na Kalunde Jamal, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post