Rais Jakaya Kikwete amewataka Watanzania kujenga utaratibu wa kupima afya zao mara kwa mara, ili waweze kutibiwa wanapogunduliwa na maradhi.
Rais Kikwete ametoa changamoto hiyo alipozungumza na wananchi na waandishi wa habari katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere,waliokwenda kumpokea wakati anarejea kutoka Marekani alikowenda kwa matibabu ya tezi dume.
Amewahakikishia watanzania kuwa afya yake imeimarika baada ya matibabu hayo na kuwataka watanzania kuwa na amani nakuendelea kumuombea.
Amewashukuru watanzania waliomtumia salamu za kumfariji na kumtakia afya njema alipokuwa katika hospitali ya Johns Hopkins iliyoko mji wa Baltimore, jimbo la Maryland nchini Marekani.
Amesema sasa ana afya njema na amani moyoni kuliko alivyokuwa awali kwani hakujua ambacho kingetokea, kwani ali amini kuwa maradhi aliyokuwa nayo ni saratani kama ilivyobainika.