MASKINI BINTI AUGUA KIFAFA AJENGEWA KIBANDA CHA KUKU,ALALA HUMO MCHANA NA USIKU

Binti wa miaka 20 aliyetambulika Riziki Haji mkazi wa Kijiji cha Kondo mkoa wa Pwani, wilayani Bagamoyo, yupo kwenye mateso makali kutokana na ugonjwa wa kifafa unaomsumbua kwa muda mrefu!
Riziki ambaye aliugua ugonjwa wa kifafa akiwa na umri wa miezi nane, amekuwa akiishi katika mazingira magumu kiasi cha kufungiwa ndani usiku na mchana.
Mtangazaji wa kipindi cha Hatua Tatu ‘Habari Ndio Hii’ cha 100.5 Times FM, Edson Mkisi Jr, alifika kijijini hapo na kushudia jinsi binti huyo anavyoishi katika mazingira ya ‘kinyama na mateso’!.
Mkisi Jr alishuhudia sehemu anayolala binti huyo ikiwa katika mazingira hatarishi kiasi kwamba yupo hatarini kung’atwa na wadudu wenye sumu kali kama nyoka, ng’e ama tangu.
 Aidha, imeelezwa kipindi cha mvua na baridi binti huyo huwa katika hali mbaya zaidi kutokana na makuti yaliyotumika kutengenezewa kibanda hayahimili hali hizo.
Akisimulia tukio hilo, jirani wa karibu na sehemu anayoishi Riziki kwa sharti na kutoandika jina lake, alisema Riziki amekuwa katika maisha mabaya kwa muda mrefu huku wazazi wake baba na mama wakitupiana mpira mtu sahihi wa kuishi nae.
“Baba wa Riziki yupo Zanzibar na anafahamu vizuri sana hali ya mtoto wake lakini wala hakuna msaada anaotuma….kuna muda mama yake aliamua kumpelekea lakini siku chache baadae alimrejesha kwa mama yake! Lakini pamoja na kumrudisha mama pia alimkataa na wasamaria wema wakamchukua na kuishi nae,” anasema jirani huyo.
Jirani huyo alibainisha kuwa akiwa anaendelea na maisha kwa msamaria huyo huku akionekana mwenye afya njema, alikuja bibi yake (mama mzazi wa mama wa Riziki) na kumchukuwa na kwenda kuishi nae Bagamoyo ambapo siku chache baadae alimrudisha kwa mama yake mzazi akidai ameshindwa kuishi nae.
Akizungumza na Mkisi Jr, mama mzazi wa Rikizi, Bi. Asma Ramadhani, alisema mtoto wake huyo awali alikuwa na afya njema lakini hajua alipatwa na tatizo gani alipompeleka kwa baba yake Zanzibar.
Kuhusu kumfungia mtoto wake ndani saa 24, alisema analazimika kufanya hivyo kutokana na hali yake huku akijitetea kwa kumuachia huru husababisha matatizo zaidi hasa anapoanguka sehemu yenye mawe.
“Zamani nilikuwa namruhusu anakwenda hata kisimani lakini sasa simruhusu tena kutokana na hali yake,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu kibanda anacholala, alisema kutokana na hali ya Riziki anashindwa kumlaza na watoto wake wadogo hivyo kwa kuhofia kuwalalalia watoto hao nyakati za usiku pindi kifafa kitakapomjia.
Hata hivyo, alikiri maisha ya mtoto wake anapolala si mazuri na kuahidi kumhamisha haraka iwezekanavyo.
Naye Juma Amani Pazi, mwenyekiti wa eneo hilo, mbali na kukiri mazingira ya Riziki kuwa mabaya, pia alisema alikuwa hana taarifa kama katika eneo lake kuna mlemavu anayeishi katika mazingira hatari kama hayo.

Na Edson Mkisi Jr

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post