YULE MTOTO ALIYEIBIWA BAADA YA MAMA YAKE KUNYWESHWA JUISI AKUTWA CHINI YA MTI,NYUZI ZA MASIKIO ZIMEIBIWA

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, David Misime

Mtoto aliyeibwa akiwa na umri wa siku nane baada ya mama yake, Teddy Bishaliza (19), kunyweshwa juisi iliyosadikiwa kutiwa dawa za kulevya akiwa nyumbani kwake eneo la Pembe ya Ng'ombe mtaa wa Chidachi, Manispaa ya Dodoma, amepatikana akiwa hai chini ya mti. 


Mtoto huyo aliibwa usiku wa kuamkia Alhamisi iliyopita na kupatikana Ijumaa ambayo gazeti hili liliandika habari za kuibwa kwake. 


Baada ya taarifa za kupotea mtoto huyo wa kike ambaye hadi habari za bibi yake, Jane Pius (39), alisema akiwa wodi namba 17 alikolazwa mama mzazi wa mtoto, Teddy, alifuatwa na askari polisi wa kike wawili na mmoja wa kiume. 


“Ilikuwa saa 2:00 asubuhi, wakanihoji kisha nikaenda nao mpaka nyumbani kwenye chumba anachoishi binti yangu ambamo yeye na mdogo wake walipewa juisi na mwanamke aliyejifanya rafiki yake kabla hajaiba mtoto usiku wa Jumatano iliyopita,” alieleza Jane. 


Alisema askari hao pamoja na mambo mengine, walishuhudia vikombe viwili ambavyo mwizi wa mtoto alivitumia kuwawekea juisi Teddy na mdogo wake, Rahel Leganga (11). 


Alisema aliachana na askari hao akarejea hospitalini kuendelea kumhudumia binti yake ambaye afya yake iliathiriwa na dawa za kulevya na kwamba saa 9:00 alasiri, alipigiwa simu na mmoja wa askari hao, akiulizwa alikokuwa na kutakiwa abaki hospitalini hapo mpaka wao (askari) wafike. 


Jane alisema saa 10:00 jioni, alifuatwa wodini na askari hao na kumtaka aongozane nao mpaka walikokuwa wameegesha gari lao, ndani ya eneo la hospitali hiyo. 


“Tulipokaribia gari wakaniambia: “Kuna mtoto ameokotwa maeneo ya Kizota Machinjioni akiwa chini ya mti, tunataka umuangalie kama ndiye mtoto wa binti yako aliyepotea.”


 “Nilipomuona nikamtambua kuwa ndiye, ingawa kuna mambo mengi yaliyojitokeza ambayo mpaka sasa sijapata majibu yake,” Jane alisema.


Alisema kabla ya kuibwa, mjukuu wake alikuwa ametobolewa masikio huku nyuzi zikiwa bado masikioni, lakini aliporudishwa nyuzi zilikuwa zimeondolewa ingawa vitundu masikioni bado vipo na kwamba kilichomsaidia zaidi kumtambua ni alama aliyozaliwa nayo pembeni kidogo ya paji la uso wake. 


UTATA WA KITOVU
Jane alisema mjukuu wake aliibwa kabla kitovu hakijakatika, lakini alipoonekana hakuwa na kitovu na kwamba alipohoji hilo, alielezwa kuwa kitovu walikipata kikiwa kando ya alikokuwa amelazwa mtoto huyo, lakini hawakumkabidhi. 


Jane alisema kuwa askari mwanaume aliwahoji askari wengine mahali kilipo  kitovu cha mjukuu wake, lakini hawakutoa jibu la kueleweka na kwamba askari huyo aliwaeleza kwamba wakitafute na kumpelekea, lakini hadi Jumamosi hakupelekewa.

UTATA WA NGUO
Jane alisema mjukuu wake aliporejeshwa alikuwa amevishwa nguo tofauti na alizovaa wakati akiibwa na kwamba Polisi waliomrejesha walisema walikuta amejichafua kwa kinyesi, hali iliyowalazimisha kumsafisha na kumvua nguo alizokutwa amevaa, ingawa hazikurejeshwa kwa wazazi wake. 


Jane alisema kuwa badala yake, alipelekwa akiwa na pande za khanga tatu na kitenge na kuwa askari alimweleza kuwa ni nguo walizozitoa wao kama sehemu ya msaada kwa mtoto huyo baada ya kumuokota chini ya mti. 


Kadhalika, kichanga hicho baada ya kurejeshwa, kilikutwa kimepakwa wanja kwenye nyusi zake na kuchorwa alama za nyota na mwezi katikati ya paji la uso tofauti na kilivyokuwa kabla ya kuibwa.


Kwa mujibu wa Jane, mwanamke anayetuhumiwa kumuiba mtoto wa Teddy, alikuwa akiwasiliana na Teddy kupitia simu yake (Jane) ya mkononi kwa (namba tunazihifadhi) ambayo inaonyesha imesajiliwa kwenye huduma ya M-Pesa kwa jina la mtu ambaye tunalihifadhi. 


Kwa mujibu wa Jane, pamoja na maelezo mengine, namba hiyo iliwasilishwa Polisi Alhamisi iliyopita wakati familia ya Teddy ikitoa maelezo kwenye Kituo Kikuu cha Polisi kuhusu tukio la kuibwa kwa mtoto huyo. 


Habari zinaeleza kwamba polisi walifanikiwa kumpata mtoto huyo baada ya kupokea simu kutoka kwa wananchi waliomuona akiwa ametelekezwa chini ya mti. 


Hadi jana hapakuwapo na taarifa zozote za kutiwa mbaroni mwa mtuhumiwa yeyote kuhusiana na tukio la kuibwa kwa mtoto huyo. 


Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, David Misime, alipoulizwa na mwandishi wa habari hizi Alhamisi iliyopita kuhusiana na tukio hilo, alisema analifanyia kazi na kwamba hawezi kuthibitisha kama mtoto huyo alikuwa ameibwa ama la. 


Juzi jioni Misime alipopigiwa simu ili azungumzie sakata hilo, simu yake ya mkononi ilipokewa na mtu aliyejitambulisha kuwa ni msaidizi wake ambaye alimwelekeza mwandishi kumpigia wakati mwingine kwa maelezo kuwa muda huo bosi wake alikuwa kwenye mkutano.

ILIVYOKUWA
Mtoto huyo wa kike aliibwa katika tukio lililotokea Mtaa wa Chidachi, Manispaa ya Dodoma na dada mmoja aliyefika nyumbani kwao na kuwapa juisi Teddy na mdogo wake, Rahel Leganga (12), ambao walilala fofofo kisha kumuiba mtoto huyo na kutoweka naye.
CHANZO: NIPASHE

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post