Hatari_POLISI WATATU WAPIGWA MAWE NA WANANCHI WENYE HASIRA HUKO KAHAMA,WALIKUWA WANAZUIA KIBAKA ASICHOMWE MOTO


Maafisa wa jeshi la Polisi wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga wakiwa katika eneo la tukio kwa ajili ya kuuchukua mwili kijana Omari Idd aliyeuawa kwa kuchomwa moto na wananchi mjini Kahama.

Mmoja kati ya vibaka 7,Omari Idd akiwa amechomwa moto na wananchi 
Maafisa wa polisi wakijiandaa kuchukua mwili wa marehemu
Mwili wa marehemu Omari Idd ukiondolewa eneo la tukio


Mwili wa marehemu ukiwekwa kwenye gari la polisi

Matukio ya wananchi kujichukulia sheria kwa kisingizio cha hasira kali yamefikia pabaya mkoani Shinyanga baada ya askari watatu wa jeshi la polisi Kahama kujeruhiwa kwa kupigwa mawe na wananchi waliojichukilia sheria mkononi wakati wakimwokoa  mwananchi aliyekuwa anashambuliwa kwa kosa la unyang’anyi muda mfupi baada ya mwenzake kuuawa kwa kupigwa fimbo na mawe kisha kuchomwa moto na wananchi hao.

 Tukio hilo limetokea Septemba mosi mwaka huu  saa moja asubuhi katika mtaa wa Bukonda moyo kata ya Zongomela wilayani Kahama.

Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga SACP Justus Kamugisha alisema askari wake watatu E.8015 D/CPL Njile,F.4301 D/C Baraka na F.107 D/C Elias walishambuliwa na wananchi kwa kupigwa mawe sehemu mbalimbali za miili yao wakati wakimwokoa Salum Juma anayetuhumiwa kwa kosa la unyang’anyi katika mtaa na kata ya Mhungula mjini Kahama.

Alisema katika kumwokoa mtuhumiwa huyo wananchi walianza kuwarushia mawe askari na kupasua vioo vya mbele vya gari la polisi lenye namba za usajili PT.3399 Toyota Landcruiser  Pick up likiendeshwa na koplo John , mali ya jeshi la polisi Kahama,na kumjeruhi koplo Njile mkono wake wa kulia,huku koplo Baraka akijeruhiwa mkono wake wa kushoto na mguu wa kulia na koplo Elias akijeruhiwa kichwani.

Kamanda Kamugisha aliongeza kuwa askari waliojeruhiwa walipatiwa matibabu katika hospitali ya wilaya ya Kahama na kuruhusiwa na hali zao zinaendelea vizuri na kwamba watu 58 akiwemo diwani wa kata ya Mhungula Josephat Matanga(52) wanashikiliwa na jeshi la polisi kwa mahojiano.

Aliwataja wengine kuwa ni Shakila Magema(37) ambaye ni mwenyekiti wa mtaa wa Bukondamoyo,Paschal Missana (44) ambaye ni kamanda wa sungusungu Mhungula na Hamis John(24) mkazi wa Bukondamoyo pamoja na watuhumiwa wengine 54.


Tukio hilo lilitokea baada ya kijana aliyejulikana kwa jina la Omari Idd(30) mkazi wa Mhungula mjini Kahama fundi washi kuuawa kwa kupigwa mawe na fimbo kisha mwili wake kuchomwa moto na wananchi hao kwa kosa la unyang’anyi wa mali.


Walioshuhudia tukio hilo waliiambia Malunde1 blog kuwa kijana huyo akiwa na wenzake 7 walivamia nyumbani kwa Juma Mkumbo(24) mkazi wa Bukondamoyo kisha kumjeruhi sehemu mbalimbali za mwili wake kwa panga katika jaribio la kunyang’anya mali usiku wa kuamkia Septemba mosi mwaka huu.

Aidha kufuatia tukio hilo wananchi walianza msako kubaini wahusika ndipo wakakamata watuhumiwa wawili kisha kuanza kumshambulia kwa mawe na fimbo kisha kumchoma moto Omari Idd.

Mashuhuda hao waliileza malunde1 blog kuwa, wakati wananchi hao wakifanya jitihada za kumchoma moto mtuhumiwa wa pili Salum Juma ndipo jeshi la polisi likafika eneo la tukio kumwokoa hali ambayo haikuwafuahisha wananchi kisha kuanza kuwashambulia kwa mawe askari polisi na kujeruhi watatu.

Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Justus Kamugusha anatoa wito kwa wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi kwa kisingizio cha hasira kali kwani ni ukiukwaji wa sheria za nchi.

Na Kadama Malunde- Shinyanga

TAFADHALI BOFYA HAPA U LIKE PAGE YETU TUKUTUMIE "HABARI" MOJA KWA MOJA KILA ZINAPOTOKEA

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com