TAZAMA PICHA_HILI NDIYO TUKIO KUBWA LEO MJINI SHINYANGA

Ndani ya ukumbi wa Karena Hotel leo mjini Shinyanga ambako kumefanyika kongamano kubwa la siku moja la wadau wa pamba nchini lililoandaliwa na Mtandao wa vikundi vya wakulima Tanzania(MVIWATA) lengo likiwa ni kujua na kupata ukweli juu ya kile kilichotokea kuhusiana na mbegu mpya ya pamba.Wakulima kutoka mikoa minne yaani Mara,Simiyu,Geita na Shinyanga wamekutana,hususani kutoka wilaya za Bukombe,Bariadi,Maswa,Kahama,Meatu,Shinyanga vijijini,Kishapu na Mbogwe.Mkutano huo pia umehudhuriwa na mbunge wa Maswa Magharibi mkoani Simiyu mheshimiwa John Shibuda (Chadema)ambaye ni mwenyekiti wa wabunge wanaotoka katika mikoa inayolima zao la pamba
Awali mratibu wa MVIWATA mkoa wa Shinyanga bwana Heri Rashid akitambulisha wadau waliohudhuria kongamano hilo la siku moja katika ukumbi wa Karena Hotel mjini Shinyanga

Wadau mbalimbali wakiwemo wakulima,wakuu wa wilaya,makatibu tawala,waandishi wa habari,wafanyakazi wa MVIWATA kutoka makao makuu wamehudhuria kongamano hilo
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Ally Nassoro Rufunga aliyekuwa mgeni rasmi kwa niaba ya wakuu wa mikoa minne inayolima zao la pamba kanda ya ziwa akifungua mkutano huo wa wadau wa zao la pamba ambapo alisema unalenga kubadilishana mawazo kuhusu mbegu za UK91 zinazozalishwa na kusambazwa na kampuni ya Quoton ambazo baada ya kupandwa katika baadhi ya maeneo hazikuota na kuwatia hasara wakulima wa zao la pamba
Katibu wa chama cha wakulima wa zao la Pamba nchini (TACOGA) bwana George Taaluma Mpanduji akifuatilia kwa makini kilichokuwa kinajiri ukumbini ambapo mambo kadha wa kadha yalijadiriwa ikiwemo suala la bei ya pamba,ambapo wadau walipendekeza pamba iuzwe shilingi 750/= kwa kilo.Pia walikubaliana mbegu zote za kipara na zenye manyoya zipelekwe kwa wakulima
Mwenyekiti wa MVIWATA mkoa wa Shinyanga bwana Charles Yona Ndugulile akizungumza katika kongamano hilo ambapo alisema pamba ni zao linalolimwa katika wilaya zaidi ya 40 katika mikoa 13 ya Tanzania bara likiajiri wakulima wanaokadiriwa kufika 500,000.Zao hilo lina umuhimu mkubwa na linaloingizia taifa fedha za kigeni na siku za nyuma kutokana na umuhimu wake zao hilo liliitwa "DHAHABU NYEUPE"

Meza kuu wakifuatilia kilichokuwa kinajiri ukumbini,ambapo ilielezwa kuwa kwa mjuda mrefu zao la pamba limekuwa likikabiliwa na changamoto nyingi kama vile tija ndogo,bei ndogo isiyokidhi gharama za uzalishaji,kilimo cha mkataba na stakabadhi ghalani ambavyo havijaeleweka vizuri kwa wakulima
 Kaimu mkurugenzi wa bodi ya pamba bwana Gabriel Mwalo akizungumza katika kongamano hilo ambapo alisema njia ya kutatua changamoto katika zao la pamba ni kilimo cha mkataba huku akiwashauri wakulima kujiunga katika vikundi na kupitia vikundi hivyo wanakikundi wataweza kununua pamba kutoka kwa wanachama na wanunuzi wa pamba watanunua pamba kutoka kwenye vikundi ili kuepukana na mawakala wasio waaminifu wanaonyonya wakulima
Wadau wakiwa ndani ya ukumbi wa Karena Hotel mjini Shinyanga

Aliyesimama ni katibu tawala mkoa wa Shinyanga Anselm Tarimo akizungumza katika kongamano hilo ambapo pamoja na mambo mengine mbali na kupigia debe kilimo cha pamba pia alisisitiza wananchi kulima mtama,alizeti na ufuta


 Aliyesimama ni bwana Joseph Ngura kutoka taasisi ya kudhibiti ubora wa mbegu Tanzania(TOSCI) akizungumza katika kongamano hilo ambapo alisema miongoni mwa changamoto wanazokabiliana nazo ni pamoja na wakulima kutozingatia sheria za mbegu kwani wengine wanachanganya pamba na mazao mengine
Aliyesimama ni mkufunzi kilimo mkuu Ukiriguru bwana Eliphas Msemo akitoa taarifa yake kuhusu utafiti alioufanya kuhusiana na mbegu zisizo na manyoya (UK91) 


Aliyesimama ni mbunge wa Maswa Magharibi mkoani Simiyu mheshimiwa John Shibuda (Chadema)ambaye ni msemaji/mwenyekiti wa wabunge wanaotoka katika mikoa inayolima zao la pamba akizungumza katika mkutano huo ambapo wakulima hawapewi nafasi ya kuzungumzia matatizo yao na badala yake viongozi wamekuwa mstari wa mbele kuzungumza wao hali inayochangia zao la pamba kuendelea kuzorota.Katika hatua nyingine aliwataka wasukuma ambao asilimia kubwa ni wakulima wa pamba kubadilika na kuwa tayari kujadili kuhusu matatizo yao na kuacha tabia ya kila kitu sawa( NDUHU TABU)

Mkulima kutoka mkoani Mara bwana Godfrey Mukiri ambaye alisisitiza wakulima waliopata hasara baada ya kulima mbegu za pamba UK91 walipwe fidia huku akiomba kuanzishwa viwanda vya nyuzi na nguo hapa nchini badala ya kutegemea viwanda vya nje vinavyosababisha bei ya pamba kushuka kila kukicha

Mkuu wa wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga Benson Mpesya akichangia mawili matatu katika kongamano hilo ambapo alitumia fursa hiyo kuwataka watendaji kutokaa maofisini waende mashambani ili kujua matatizo yanayowakabili wakulima

Kushoto ni mbunge wa Maswa Magharibi mheshimiwa John Shibuda akifurahia jambo katika ukumbi wa Karena Hotel mjini Shinyanga leo

Aliyesimama ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Ngassa Mboje akichangia mawili matatu katika kongamano hilo ambapo alisema bodi ya pamba chanzo cha matatizo ya wakulima wa zao la pamba ambao mara nyingi wamekuwa wakilima pamba bila kupata faida 

Kongamano linaendelea.Changamoto zilizotajwa kuzorotesha zao la pamba ni pamoja na uchafuzi wa pamba,uuzaji wa pamba ghafi nje ya nchi,pembejeo,kilimo cha kutegemea mvua,mabadiliko ya tabia nchi,udanganyifu(wizi) katika mizani na wakulima wa pembezoni kutokuwa na taarifa za kutosha kuhusu zao la pamba.

Mkulima kutoka Meatu bwana Bonane wa Bonane Kasimbagu akielezea jinsi alivyopata hasara baada ya kulima mbegu za pamba zisizo na manyoya huku akiomba wakulima waliopata hasara kulipwa fidia-Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog Shinyanga

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527