Hujafa Hujaumbika_Msaada!! UGONJWA WA AJABU WAMTESA KIJANA HUYU

 Kijana Lawrent Lawrian, akiwa na uvimbe wa ajabu kichwani mwake.

Lawrent Lawrian, 42 (pichani), ni mkazi wa Kijiji cha Nyakisogo, Wilaya ya Biharamlo, mkoani Kagera, amekuwa mwenye huzuni na kukosa raha kwa muda wa miaka 35 kutokana na gonjwa la ajabu linalomtesa ambalo limemsababishia mambo mengi ikiwa ni pamoja na kutoendelea na masomo.

 Gonjwa hilo la ajabu ni uvimbe kama nundu kichwani wenye uzito wa kilo 3, ulimuanza akiwa darasa la kwanza.

Akielezea zaidi kwa njia ya simu hivi karibuni Lawrent alisema: “Gonjwa hili lilianza kama kauvimbe nikiwa na umri wa miaka saba, wakati huo nilikuwa na wazazi wote na ilipofika mwaka 1992 baba akafariki dunia. 

“Nikabakia na mama tukawa tunaishi kwa kutegemea kilimo cha kawaida, nilikuwa nikienda shule lakini ilifikia hatua nilishindwa kutokana na maumivu na manyanyaso.

 “Darasa la saba nilimaliza kwa tabu sana, kwani wanafunzi wenzangu walikuwa wakinicheka na kunitenga, licha ya kuadhibiwa na walimu lakini hawakuacha tabia yao.

“Kutokana na hali hiyo, nilishindwa kuendelea na masomo kwani nilikuwa nikifungiwa ndani ili kunipunguzia kero toka kwa wenzangu.
Kijana Lawrent Lawrian akiuguza uvimbe.

 “Nilikaa kwa kujificha hadi nilipojiona mkubwa nikaamua kuoa, sasa nina watoto sita wanaonitegemea.

“Kwa upande wa matibabu baada ya uvimbe kuwa mkubwa nilipelekwa kwa padri mmoja katika Hospitali ya Wilaya ya Biharamulo lakini hawakugundua tatizo kutokana na kutokuwa na vifaa vya kumpimia. 

“Baadaye kuna madaktari Wazungu walifika katika Hospitali ya Bukoba nikaenda, waliponipima walisema ni uvimbe wa kawaida lakini hawakuweza kunitibu. 

“Ilibidi nikae nyumbani, maumivu yalizidi kuongezeka nikawa nashindwa kupata usingizi, nikalazimika kwenda Hospitali ya Mgana, nilifanyiwa vipimo, nao walisema ni uvimbe wa kawaida ambao unatakiwa ufanyiwe upasuaji na nikaambiwa gharama yake ni shilingi milioni moja na laki sita, nikashindwa kwa kuwa sina fedha hizo. 

“Kwa sasa uvimbe huu umekua mkubwa sana na ni mzito na umenifanya nishindwe kwenda shambani, nimekuwa mtu wa kulala, familia yangu nayo inapata shida.

 “Mtoto wangu wa kwanza kati ya sita yupo kidato cha pili na wote wamekuwa wakimtegemea mama yao anayewatunza kwa kipato kidogo kinachopatikana kutokana na kilimo cha jembe la mkono.

“Nawaomba wasamaria wema wanisaidie kupata fedha za matibabu ili kuokoa maisha yangu kwa kuwasiliana nami kwa namba 0714-533 430.”

via>>matukiotz

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527