Askofu Kakobe aliyasema hayo juzi kufuatia tukio hilo lililojiri siku tano kabla ya Sikukuu ya Pasaka ambapo mwezi wote ulipatwa (lunar eclipse) na kuwa mwekundu kama damu, tukio ambalo pia litatokea tena mwakani.Kufuatia tukio hilo lenye kuogofya, baadhi ya mitandao ya kijamii duniani kote imekumbushia maneno ya manabii mbalimbali lakini zaidi kutoka kwenye Biblia wakisema mwisho wa dunia sasa ni dhahiri.
MSIKIE KWA UNDANI
“Kinachotakiwa kwa watu sasa ni kuacha maovu na kumrudia Mungu. Ni wajibu wa kila mtu kujiweka tayari kwa kuokoka kwani bila kufanya hivyo watakaokutwa katika dhambi watatupwa jehanamu,” alitahadharisha Askofu Kakobe.
Aliongeza kuwa, dalili zote za mwisho wa dunia zilizotajwa katika Biblia ziko wazi kwa sasa, kama vile hilo la mwezi wa damu, kuzuka kwa manabii wa uongo, vita ya nchi na nchi na ukoo kwa ukoo lakini akasema hajui ni kwa nini watu hawataki kuokoka.
NAYE MAMA RWAKATARE
Naye Mchugaji wa Kanisa la Assemblies of God ‘Mikocheni B’ la jijini Dar, Mama Getrude Rwakatare alikiri kulijua hilo la mwezi kuwa wa damu na kusema katiba Biblia, Luka 21:25 Mungu amefafanua kuwa kuna dalili mbalimbali zitajitokeza siku za mwisho wa dunia na sasa zinaanza kuonekana, akawataka watu kuomba bila kuchoka.
“Dalili nyingine ni mataifa kupigana, upendo wa wengi kupoa, manabii wa uongo kuibuka na kadhalika. Haya tunayaona sasa, hivyo watu wote tumrudie Mungu,” alisema Mama Rwakatare.
NABII SUGUYE PIA
Uwazi lilibahatika kuzungumza na Nabii Nicolaus Suguye wa Kanisa la Huduma na Neno la Upatanisho ambaye alisema dalili za mwisho wa dunia ni nyingi ambazo ni mataifa kupigana, kukosa uhusiano mzuri na kuzuka kwa manabii wa uongo.
NABII GEODAVIE AJUAVYO YEYE
Uwazi lilikwenda mbele zaidi kwa kuzungumza na kiongozi wa Kanisa la Ngurumo za Upako lenye makao makuu jijini Arusha, George David ‘GeoDavie’ ambapo alikuwa na haya ya kusema:
“Suala la kupatwa kwa mwezi na kuwa damu ni ishara ya mwisho wa dunia lakini nasisitiza kuwa pia ni jambo la kisayansi zaidi.”
Alizidi kusema kuwa kilichoandikwa kwenye Biblia, Luka 21:25 (Tena kutakuwa na ishara katika jua na mwezi na nyota na katika nchi, dhiki ya mataifa wakishangaa kwa uvumi wa bahari na msukosuko wake) lazima kikubalike na kila anayemwamini Mungu.
IMANI MWAKYOMA WA TAG
Mchungaji Imani Mwakyoma wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) Magomeni jijini Dar, yeye alisema kupatwa kwa mwezi na kuonekana wa rangi ya damu ni mafundisho ambayo watumishi wa Mungu wamekuwa wakiihubiri kila kukicha.
“Tumekuwa tukihubiri kwa muda wa miaka kumi sasa kwamba mwisho utafika pale tu ishara ya anga itakapoanza kuonekana, mwezi kuwa wa damu na jua kuwa giza, siku hizi kila mara jua linapatwa na kuwa giza, bado nini sasa hapo? Watu wamrejee Mungu,” alisema Mchungaji Mwakyoma.
ASKOFU MALASUSA, KARDINALI PENGO
Baadhi ya waumini wa kanisa la Romani Katoliki linaloongozwa na Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo na Kanisa la KKT linaloongozwa na Askofu Dr. Alex Gerhaz Malasusa, walisema watumishi hao wa Mungu mara kwa mara wamekuwa wakihubiri watu kutubu kwa kuwa siku za mwisho wa dunia zipo dhahiri kwa sasa.
MCHUNGAJI WA MAREKANI
Naye John Hagee, Mchungaji wa Kanisa la Cornerstone, San Antonio, Texas Marekani na mwanzilishi wa muunganiko wa Wakristo nchini Israeli alishawahi kutoa kitabu akiongozwa na taasisi ya uchunguzi wa anga za juu ya nchi hiyo, NASA kwa kufanya makadirio kupitia historia ambapo aliandika uhusiano wa moja kwa moja kati ya kupatwa kwa mwezi na kuwa mwekundu na utabiri wa Waisrael na wanadamu wote.
NI KARIBU NA PASAKA TU?
Katika kitabu hicho, Mchungaji Hagee aliandika kwamba, zaidi ya miaka 500 iliyopita kupatwa kwa mwezi wa damu kulitokea siku ya kwanza ya Sikukuu ya Pasaka mara tatu tofauti.’
Hata Aprili mwaka huu, mwezi huo ulipatwa na kuwa mwekundu kuelekea Sikukuu ya Pasaka na itatokea tena mwakani kipindi cha Pasaka.
LAZIMA WATU WAJUE ISHARA
Mchungaji Hagee alifafanua kwamba kupatwa kwa mwezi ni lazima watu, hasa Wakristo waelewe ishara hizo. Alisema katika Biblia, Joel: 2 na Matendo ya Mitume: 2 vyote vimeandika tukio hilo kwamba ndiyo mapito ya dunia kuelekea mwisho wake.
BAADA YA MATUKIO HAYA
Kwa mujibu wa Markell, mchambuzi wa mambo ya sayansi, kupatwa kwa mwezi na kuwa wa damu kutatokea tena katika mpangilio wa Oktoba 8, 2014, Aprili 4, 2015 na Septemba 28, 2015!
IMANI YA KIKRISTO
Hata hivyo, Markell anasema kuwa Wakristo wengi wanaamini maneno ya kale kwamba kupatwa kwa mwezi ni dalili ya ujio wa pili wa Kristo na hivyo kusababisha hofu miongoni mwa wale ambao hawajui maana halisi japo maelezo ya kisayansi yanafafanua jambo hili.
Alisema kimsingi, rangi ya mwezi ni nyekundu ambayo ipo katika anga ya dunia na kama dunia haina anga, moja kwa moja mwezi utafunikwa na giza.
Markell ambaye anaamini kwamba shetani yupo nyuma ya harakati za maendeleo, anasema hakuna mtu anayejua ishara za mwezi lakini alipendekeza kuwa dunia inapaswa kubashiri kwa habari mbaya.
via__Uwazi