Noumaaa mtupu!! MADIWANI SHINYANGA WAGEUKA MBOGO, WADAI WAWEKEZAJI WA KICHINA NI WALAGHAI,WANAFANYA KAZI KWA UJANJA UJANJA,KILA MARA WANAKIMBILIA KWA RC


Baraza  la madiwani katika manispaa ya Shinyanga limeitahadharisha serikali kuwa makini na wawekezaji  wa kigeni wanaoingia nchini na kuanza kuendesha shughuli zao kijanja kijanja kwa kushindwa  kufuata masharti ya mkataba na kubadili matumizi bila kushirikisha jamii ya eneo husika iliyotoa eneo.

Hayo yamesemwa jana na mjumbe wa kamati ya miundombinu katika baraza hilo ambaye ni diwani wa kata ya Chamaghua  Morice Mghin,wakati akitoa taarifa ya ziara ya kamati hiyo iliyotembelea  kiwanda cha nguo ,gineri ya kuchambua pamba na kiwanda cha ngozi vyote vikiwa na wawekezaji wa kigeni kutoka nchini china.

Mghin alisema makubaliano yaliyopo kwa wawekezaji hao katika kiwanda cha nguo cha N’ghelegani  ni kuanzisha shule itakayotoa elimu kwa wakulima wa pamba lakini hawajafanya hivyo.

Katika hatua nyingine alisema wawekezaji hao wanatakiwa kujenga kiwanda cha nguo katika eneo hilo la Nh’elegani  na badala yake wamejenga kiwanda cha kuchambua nyuzi ambazo zitasafirishwa kwenda nchini kwao China.

Aidha alisema katika kiwanda cha Ibadakuli makubaliano ni kujenga kiwanda cha kusindika nyama lakini kinachoendelea mpaka sasa ni shughuli za kusindika ngozi kinyume na makubaliano  wakati wanaomba kupatiwa ardhi kwa ajili ya uwekezaji.

“Wawekezaji hawa hawafuati maelekezo ,wanakiuka masharti,wengi wao ni walaghai,kamati hii pia imeona hata mazingira ya kazi kwa wafanyakazi, siyo mazuri kutokana na kukosa vifaa vya kujikinga wakati wakifanyakazi,wananchi wetu hawathaminiwi”,alisisitiza.

“Kwa hali hii ni bora manispaa ikaacha kupokea wawekezaji wanaoingia kwa njia za panya,inatakiwa mwekezaji anapokuja azingatie masharti na makubaliano yote lakini hawa wenzetu hawafanyi hivyo hata kama kuna mabadiliko ni vema wakashirikisha uongozi wao wanajiamlia tu”aliongeza Mughin.

Kwa upande wake mwenyekiti wa baraza hilo ambaye ni naibu mstahiki meya wa manispaa hiyo David Nkulila,alisema madiwani ndiyo wenye maamuzi na mamlaka ya kupanga mambo yanayohusu halmashauri, lakini wawekezaji hao wao wanachojua ni viongozi wa kubwa akiwemo mkuu wa mkoa wakati wako chini ya manispaa hali inayoleta mgongano.

Alisema ni vyema pia viongozi wakubwa kama mkuu wa mkoa wakafuata utawala bora kwani hali hiyo inasababisha usumbufu hata kwa wataalam wa manispaa pindi wanapokwenda kudai  mapato kwa wawekezaji hao kwani wawekezaji hao wamekuwa hawawajali,wao kiongozi wanayemjua ni mkuu wa mkoa tu.
“Kwa kweli,siyo kwamba hatupendi wawekezaji,hapana,tatizo hawa wawekezaji wa kichina wanafanya kazi kwa ujanja ujanja,maafisa wetu wanahangaika sana,wanashindwa kuelewana hadi lugha,ukiwafuata wanadai hawajui Kiswahili,ukionekana unajua Kiingereza nacho wanasema hawajui”,aliongeza Nkulila.

Naye kaimu mkurugenzi wa manispaa hiyo Dismas  Minja,alisema  ni vyema serikali ikawa macho na wawekezaji walaghai,huku ikitambulika kuwa manispaa ndiyo inamiliki ardhi hivyo inawajibu wa kufuatilia jinsi inavyotumika.

Aidha alisema wawekezaji wanapaswa kufuata sheria na taratibu zote na kuwataka  viongozi  pamoja na baraza la madiwani ,kuwa macho kwani ardhi inayochukuliwa na wawekezaji hao kuwa ni kubwa halafu wananchi hawanufaiki nayo huku wawekezaji wakishindwa kulipa mapato serikalini.

Na Kadama Malunde-Shinyanga

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post