NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI AKUTANA NA WAFUGAJI WILAYANI KISHAPU

 
Ikiwa ni  chache tu baada ya kutokea mauaji ya watu watano na wengine zaidi ya 20 kujeruhiwa wakati wa mapigano ya wafugaji na wakulima katika eneo la mpaka kati ya wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga na Igunga mkoani Tabora  kutokana na mgogoro wa ardhi,imeelezwa kuwa ugomvi huo pia umetokana na wananchi kugombania maji ya mto Manonga uliopo katika eneo hilo.

Akizungumza juzi kwenye mkutano wa hadhara na wafugaji wa kabila la Kitaturu wilayani Kishapu naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi nchini Kaika Telele baada ya kutembelea eneo la mgogoro huo na kujionea jinsi machafuko yalivyotokea alisema kila upande umekuwa ukiutupia lawama upande wa pili kwamba wao ndiyo wakorofi.
Alisema baada ya kukutana na pande zote mbili na kuzungumza nao amebaini kwamba sababu nyingine ya kutokea kwa mgogoro huo ni wananchi kugombania maji ya Mto Manonga uliopo katika eneo hilo ambapo wakulima na wafugaji wamekuwa wakivutana.
 “Wakulima wanatumia maji ya Mto Manonga kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji  wamekuwa wakidai kuwa wafugaji wanachafua maji hayo kwa kujaza vinyesi vya ng’ombe,na wafugaji nao wanadai kuwa wakulima wanatumia maji mengi kumwagilia mashamba yao na hivyo kuna hatari ya kukosa maji ya kunyweshea mifugo yao”,alifafanua waziri Telele
Waziri Telele baada ya kutembelea eneo hilo la mgogoro na kuzungumza na pande zote mbili  za wakulima wa Igunga na wafugaji wa Kishapu ambapo kila wilaya imekuwa ikisema eneo hilo ni lao, ataunda tume ya wataalamu kulichunguza tatizo la mgogoro huo pamoja na kupima hekali ya  eneo lote na kuligawa katikati.
“Tarehe 4 mwezi huu nimeongea na wafugaji wa Igunga kuhusu eneo hilo na leo naongea na nyie wafugaji wa Kishapu,na kila upande unasema upo sahihi kutumia eneo la mpaka huo,suala hili nalichukua na nitaliundia tume ya wataalamu ili kufika katika eneo la mgogoro kwa kupima eneo lote na kuligawa kisheria kila wilaya ipate upande wake”,alisema Telele
 Aidha alizitaka kamati za ulinzi na usalama za pande zote mbili ziendelee kuimarisha ulinzi wa maeneo yao na kuwatuliza wananchi wazingatie maelekezo ya kutovuka Mto Manonga mpaka hapo Serikali itakapo tatua tatizo hilo kisheria ilikuzuia machafuko yasitokee tena.
 
Naye mwenyekiti wa wafugaji katika kijiji cha Magalata wilayani Kishapu Jidonye Majuluga  alisema  tume hiyo inatakiwa kuundwa haraka iwezekanavyo ikiwezekana ndani ya mwezi huu kwani wakulima bado wanavuka mto huo na kuingia katika eneo la wafugaji hivyo machafuko ya uvunjifu wa amani yanaweza kutokea tena muda wowote.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post