Kumbe kuna maaskofu Feki!!! WANAONUNUA UASKOFU WASHTUKIWA,WADAIWA KUTOA FEDHA WAPATE CHEO,SOMA ZAIDI HAPA

Askofu Mkuu Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk Jacob Chimeledya ameonya tabia ya makasisi kutoa fedha ili kununua Uaskofu kwani hiyo ni aibu. 

Alisema hayo jana mjini Dodoma wakati wa ibada ya maziko ya aliyekuwa Askofu wa Dayosisi ya Central Tanganyika, Godfrey Mhogolo yaliyofanyika kwenye viwanja vya kanisa hilo.

Alisema sasa kumekuwa na tabia ya kutafuta uaskofu wa kununua na watu wamekuwa wakitoa fedha ili wapate cheo hicho.

"Wakati mwingine watu wanatafuta na kununua uaskofu ni kitu cha aibu, kwani kasisi anatafuta kwa gharama yoyote ili awe askofu," alisema.

Alisema sasa wakati wa kujaza nafasi hiyo utafika ili kanisa lisonge mbele na mchakato wa uchaguzi utakapoanza wataomba ili apatikane kiongozi aliyeitwa na Mungu.

"Sisi tunasikia tayari mmeshaanza kampeni kama zile wanavyogombea katika siasa, lakini ndani ya kanisa hatunadi sera ni kuomba uongozi wa roho mtakatifu ili apatikane mtu wa kujaza nafasi hiyo," alisema.

Kauli ya Askofu mstaafu Kwa upande wake, Askofu Mkuu Mstaafu wa Kanisa hilo, Donald Mtetemela pia aliwataka wachungaji kuacha vita ya madaraka kutokana na kanisa kuingiliwa na tabia za watu wenye tamaa za kutaka vyeo.

Alisema baadhi ya watu wenye kupenda vyeo hatari wameanza kufikiri ni nani atashika nafasi hiyo alisema sasa chuki na mioyo ya kuchafuana itainuka jambo ambalo si la kumpendeza Mungu.

Aliwataka viongozi hao kulihurumia kanisa kwani vyeo ni vingi, lakini kuna mtu moja tu ambaye kanisa linamhitaji.

"Tuinue watumishi ambao watasimamia kanisa lao vizuri, mtafuteni mchungaji ambaye ataendeleza kwa uaminifu kanisa la Mungu," alisema .

Mtetemela alisema Askofu Mhogole alikuwa ni mtu wa kuthubutu, kwani aliweza kuwekea mikono wanawake wawe wachungaji pia alikuwa mtu wa kujadiliana sana na kanisa limempoteza kiongozi mwenye mapenzi mema na watu.

Alisema wakati mwingine kanisa limepata viongozi wanaoharibu kazi za Mungu na kutaka waumini waombe ili Mungu aipatie dayosisi hiyo kiongozi mwingine mwaminifu.

"Wachungaji watulie, Bwana anawaona. Tuache vita ya madaraka ndani ya kanisa," alisema na kuongeza kuwa, Askofu Mhogole alianza kazi kama mhudumu wa ofisi, alifanya usafi, kupika chai alipokea simu na kupeleka barua posta.

"Mahali popote Mungu anapokuweka ana sababu zake Mungu anapotaka kukuandaa wewe anakuweka kwenye kazi anayoona inafaa," alisema.

Alisema ni muhimu kwa watu kutumia fursa wanazopata katika kazi kwa kuinua wengine na si kupata cheo na kutazama namna ya kukomoa watu wengine.

Waziri Mkuu Pinda Kwa upande wake Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema, Askofu Mhogolo alikuwa ni kiongozi makini kwani aliweza kusimamia parishi 265 zenye makasisi zaidi ya 300 huku waumini wa dayosisi ya kati wakiwa zaidi ya 600,000.

Alisema kazi nyingi alifanya kwenye sekta ya afya, eli
mu na aliitumikia jamii na hata kukea na kusomesha yatima jambo ambalo atazidi kukumbukwa.

 "Uovu kila mmoja ana wa kwake, lakini wema si kila mmoja anao, lakini changamoto kubwa ni kwa yule atakayevaa viatu vyake kufanya mema au zaidi ya yale aliyokuwa ameyafanya," alisema.

Maneno ya Malecela Kwa upande wake Waziri Mkuu mstaafu John Malecela alisema atamkumbuka Askofu Mhogolo kwa mema mengi ikiwemo tukio la kumfungisha ndoa na Anne Kilango miaka 11 iliyopita.

Alisema askofu huyo alikuwa ni mpenda maendeleo na wakati akianza kazi kanisa lilikuwa likitegemea sana wafadhili, lakini akasaidia sana kanisa kujitegemea.

Alisema sasa kanisa lina mali zenye thamani ya Sh bilioni nane. Malecela alisema aliwahi kumsihi askofu huyo ili hospitali ya Mvumi inayomilikiwa na kanisa hilo iwe hospitali ya Teule ya Wilaya ya Chamwino alikubali na jambo hilo likafanyika.

"Alikuwa ni mtu aliyejali na msikivu hatutamsahau daima," alisema Mchungaji Noah Masima alisema alilelewa na kukua pamoja na marehemu askofu Mhogolo ambaye alipofikisha miaka 16 wazazi wake wote walifariki.

"Tulikuwa marafiki wa rika moja tulienda shule pamoja darasa moja, michezo ya watoto pamoja tulitumia ulimbapo kutafuta ndege porini, tukapigana mieleka baadaye nikachaguliwa kwenda Mvumi Middle School yeye akaenda shuleni Chilonwa," alisema.

Alisema alipofikisha miaka 16, Mhogolo alifiwa na wazazi wake wawili kwa nyakati tofauti na kulazimika kuishi na wadogo zake wote ndipo alipopata kazi Mackey House kisha akaenda masomoni Australia.

"Alikuwa ni mtu mwenye msimamo aliitetea kweli, muadilifu tangu udogo wake hapa alipokufa alipenda sana yatima, alijali wajane na wastaafu," alisema. Askofu Mhogolo ameacha mjane, watoto watatu na wajukuu kadhaa.
Via>>Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post