HAYA NDIYO MADHARA YA UNENE KWA WAJAWAZITO NA WATOTO



Unapaswa kujua kuwa, wanawake wenye uzito wa kupitiliza (obese women) wakiwa wajawazito wanakabiliwa na hatari ya kupata madhara makubwa.
Madhara hayo ni kama haya yafuatayo, kupata ugonjwa wa kisukari cha ujauzito ambacho ni hatari kwa maisha yake.
Mjamzito pia anaweza kupata matatizo ya shinikizo la damu wakati wa ujauzito pamoja na kifafa cha mimba ambacho ni hatari sana kama kinamtokea wakati wa kujifungua. Vilevile wajawazito wanene kupindukia wanaweza kupata tatizo la kujifungua kwa njia ya upasuaji kitabibu huitwa Caesarean section.
Lakini pia mjamzito mnene kupindukia anaweza kupatwa na tatizo la mtoto aliye tumboni kutopata hewa vizuri wakati wa ujauzito, kitaalamu huitwa Fetal distress.
Matatizo ya unene kwa watoto
Taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO), inatahadharisha juu ya unene wa kupindukia kwa watoto. Wamesema kwamba watajaribu kupunguza kutumiwa vyakula holela (junk food) kwa kupiga marufuku matangazo ya vyakula hivyo katika vyombo vya habari na kwa kutumia mabango mitaani na mawaziri wa afya wa nchi mbalimbali wamepewa angalizo hilo.
Viwanda vya vyakula na vinywaji vimetakiwa kuongeza udhibiti wa aina zote za mauzo ya vyakula kwa watoto na wauzaji vyakula vya watoto wadogo pia wametakiwa kuacha kuzalisha na kuuza vyakula ambavyo si vizuri kwa afya ya watoto.
WHO imesema kwamba, unene wa kupindukia kwa watoto unaongezeka duniani kote. Shirika hilo limeshauri kwamba, wazazi wanapasa kupunguza muda wa watoto wao kutazama televisheni.
Limeshauri pia watoto kubanwa kutumia vyakula holela na vinywaji vyenye sukari nyingi mashuleni na sehemu za michezo ya watoto, hili walimu wanapaswa kulizingatia.
USHAURI
Watoto waepuke kula vyakula vyenye sukari nyingi na vyenye mafuta mengi na ni vema kwa wajawazito kufanya mazoezi na kuepuka vyakula vyenye mafuta mengi. Jinsi ya kufanya mazoezi tulishaeleza kwenye makala zetu zilizopita katika safu hii.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post