WAKUU WA MIKOA WATAKIWA KUACHA KUTUMIA VITISHO BALI WAONGOZWE NA BUSARA

 
Baadhi ya wadau wa zao la Pamba katika mikoa ya Shinyanga na Mwanza wamewaomba wakuu wa mikoa na wilaya kutumia busara zaidi pale wanapowahamasisha wakulima na wanunuzi wa zao hilo kuhusiana na utekelezaji wa mpango wa kilimo cha mkataba badala ya kutumia vitisho.
 
Ombi hilo limetolewa juzi na baadhi ya wawekezaji katika zao la Pamba katika mikoa ya Shinyanga na Mwanza kufuatia tukio la hivi karibuni la mkuu wa mkoa wa Geita, Magalula Said Magalula kutoa amri ya kuwekwa ndani kwa wawakilishi wa makampuni matatu ya ununuzi wa pamba katika mkoa wake.
 
Wakizungumza na waandishi wa habari mjini Kahama baadhi ya wamiliki wa makampuni ambayo wawakilishi wao waliwekwa ndani kwa masaa manne kutokana na agizo la mkuu huyo wa mkoa walidai kuwa kitendo alichokifanya kilikuwa ni kinyume na dhana nzima ya utawala bora.
 
Wawakilishi waliowekwa ndani hivi karibuni kwa amri hiyo ya mkuu wa mkoa wakati wa kikao cha wadau wa zao la pamba mkoani Geita ni pamoja na mwakilishi wa kampuni ya Fresho Investment Ltd., Kahama Oil Mill Ltd. na ICK Cotton Co. Ltd.
 
Walisema suala la kilimo cha mkataba ambacho kina lengo la kumkomboa mkulima aweze kunufaika na kilimo chake cha zao la pamba linaungwa mkono na kila mdau wa zao hilo isipokuwa kinachotakiwa kabla ya utekelezaji wake ni kuondoa changamoto zote zilizobainika katika kikao cha wadau kilichofanyika jijini Mwanza Oktoba 20, 2013.
 
Mmoja wa wamiliki wa makampuni ya ununuzi wa pamba mjini Kahama (jina tunalo) alisema kitendo alichokifanya mkuu wa mkoa wa Geita ni cha kusitikisha na kinaweza kusababisha watu washindwe kutekeleza vyema mpango huo wa kilimo cha mkataba iwapo wataamua kuutekeleza kwa shinikizo la viongozi wakuu wa serikali badala ya hiari yao wenyewe.
 
“Binafsi sikuridhishwa na hatua ya mkuu wa mkoa, kutumia vitisho kwa lengo la kututisha siyo suluhisho la watu kutekeleza kilimo cha mkataba, kuweka ndani watu ni kuwadhalilisha, na ikiwezekana tunaweza kumpeleka mahakamani ili atusafishe, maana kitendo chake kimeonesha sisi siyo waaminifu kwa wakulima tunaofanya nao kazi,”
 
“Ametoa agizo watu wamewekwa ndani, baada ya masaa manne polisi wamewaachia kutokana na kukosa shitaka la kuwafungulia, sasa huu siyo utawala bora, kilimo cha mkataba kitafanikiwa vizuri kwa watu kuelimishwa kwa kina lakini pia ni pamoja na kuondoa changamoto zote zilizojitokeza wakati wa majaribio yake,” alieleza mdau huyo.
 
Hata hivyo kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Geita, Magalula Said Magalula akizungumzia tishio la kutaka kupelekwa mahakamani kama ilivyodaiwa na baadhi ya wawekezaji hao alisema hiyo ni haki yao ya kikatiba iwapo wataamua kufanya hivyo na yeye atakwenda kutoa ushahidi wake kwa nini alitoa amri hiyo.
 
“Kama hawa wenzangu wataamua kunipeleka mahakamani, hiyo ni haki yao kabisa, lakini agizo langu lilitokana na wao kukiuka makubaliano tuliyokuwa tumekubaliana katika kikao cha wadau wote wa zao la pamba kilichofanyika hivi karibuni, walipewa viuatilifu wakiviuze kwa wakulima kwa mkopo wao waliuza kwa fedha taslimu,”
 
“Lakini hata kama walikuwa na tatizo katika kusambaza viuatilivu hivyo kwa njia ya mkopo basi ilikuwa ni wajibu wao waje ofisini wanieleze tatizo, hawakufanya hivyo waliuza kwa fedha taslimu lakini hata hivyo fedha za mauzo hawakuzirejesha bodi ya pamba, kitendo chao kilisababisha baadhi ya wakulima wakose viuatilivu kwa vile hawana fedha,” alieleza Magalula.
 
Kwa upande mwingine mkuu huyo alishindwa kufafanua iwapo wawekezaji hao walifikishwa mahakamani baada ya kutoa agizo wakamatwe na wawekwe ndani ambapo alisema anayepaswa kutoa jibu iwapo walipelekwa mahakamani au hawakupelekwa ni kamanda wa polisi wa mkoa wa Geita.
 
Hata hivyo taarifa kutoka Jeshi la Polisi mkoani Geita zilieleza watuhumiwa wote waliokuwa wamekamatwa waliachiwa huru baada ya kukosekana kwa kifungu cha sheria ambacho kingetumika kuweza kuwafikisha mahakamani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post