Stori ya Jamaa Kubadilika kuwa ALBINO!!! UTSS YATOA UFAFANUZI,KUMBE NI UGONJWA UNAJULIKANA KWA JINA LA VITILIGO,SOMA ZAIDI HAPA

 Adai Metakelfin imemgeuza kuwa Albino, Msikilize hapa akieleza ilivyokuwa

Na Edward Kondela – Mwandishi wa habari (UTSS)
  
Shirika la Under The Same Sun (UTSS) limetoa ufafanuzi wa taarifa iliyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari hapa nchini,ukiwemo mtandao huu wa Malunde1 blog ikimhusu mkazi mmoja wa mkoa wa Tabora anayedaiwa kupata albinism ukubwani kuwa hana hali hiyo bali ana ugonjwa wa vitiligo.

Akizungumza katika ofisi za UTSS jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo hapa nchini Vicky Ntetema, ameitaka jamii kuelewa kuwa albinism ni hali ya kurithi kutoka kwa wazazi wote wawili na kwamba hauwezi kupata kwa kuathiriwa na dawa.

“Haiwezekani mtu azaliwe bila albinism halafu aje apate albinism ukubwani, ni kwamba baba na mama wanakuwa na vinasaba vinavyokuwa na albinism na vinapokutana wakati wa kutunga mtoto ndipo mtoto mwenye albinism anazaliwa hivyo ni lazima urithi kutoka kwa wazazi wako” amesema Vicky Ntetema.

Kwa upande wake Dokta Jeff Luande mtaalam wa magonjwa ya saratani na mwenye uzoefu mkubwa juu ya albinism kutoka Hospitali ya Ocean Road jijini Dar es Salaam, amesema kukosekana kwa taarifa sahihi kunaweza kumsababishia mgonjwa kutofahamu hali yake na hata kushindwa kupata matibabu au ushauri.

“Ngozi kubadilika kuwa nyeupe, kwa mtu wa kawaida atajua ni albinism lakini kutumia hili neno kwa huyu Bwana Masokola siyo sahihi, yeye amepata ugonjwa unaoitwa vitiligo mara nyingi huwa yanatokea madoadoa meupe kwenye ngozi” amebainisha Dokta Luande.

Amefafanua kuwa ugonjwa huo huweza kutokea kutokana na matumizi ya dawa mbalimbali zikiwemo zenye sulphur japokuwa ni kesi chache sana kwa mtu kubadilika mwili mzima kama Bwana Masokola, ambaye huenda alipata ugonjwa huo baada ya kutumia dawa yenye sulphur iliyoharibu mfumo wa kutengeneza rangi asili ya mwili.

Ameongeza kuwa mtu aliyepata ugonjwa wa vitiligo kama Bwana Masokola, anapaswa kujikinga na jua kama mtu mwenye albinism ili asipate saratani ya ngozi kwa kuwa ngozi yake haina uwezo wa kuhimili miale ya jua.

Hivi karibuni katika mitandao ya kijamii na gazeti moja hapa nchini limemripoti Bwana Hafidh Masokola Damson mkazi wa mkoa wa Tabora anayedai kupata albinism baada ya kunywa dawa aina ya Metakelfin hali iliyosababisha baadhi ya maswali kwa jamii.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post