WAJAWAZITO WAJIFUNGUA KWA KUTUMIA MWANGA WA TOCHI YA SIMU NA CHEMLI -SHINYANGA

 
Kituo  cha afya cha Ikonongo kilichopo kata ya Salawe  wilayani Shinyanga  kinakabiliwa na changamoto mbalimbali  ikiwemo ukosefu  wa huduma ya maji na  nishati ya umeme hali ambayo inawalazimu  akina mama wajawazito kutumia tochi  ya simu au taa wakati wa kujifungua huku watoto wanaougua kuchanganywa na wakubwa.
Baadhi ya wananchi wa kata hiyo  walieleza kuwa   kumekuwepo na tatizo la kupata huduma iliyo bora kwani  vifaa vya kupimia maradhi yanayowasumbua hakuna, mama wajawazito kutumia  mwanga wa simu ya tochi wakati wa kujifungua , wamalizapo kujifungua nguo  zao hulazimika  kwenda kufulia  kwenye malambo  sehemu ambayo maji hutumiwa na watu wote.
Walisema  wamekuwa wakipata  shida ya kupata huduma katika kituo hicho  kwani hakuna  maji  hivyo wanapokwenda kujifungua hulazimika kwenda na maji yao.
 
Mwenyekiti wa kijiji cha  Azimio  Twiga  Mashimba  alisema kuwa  kituo hicho kinahudumia  vijiji zaidi ya vitano  na kata nne  ambazo ni Mwakitolyo,Mwenge na Salawe  ambapo kijiji chake kina watu  zaidi ya 3000  na kwamba kituo kinakabiliwa na changamoto ya uhaba wa wodi  ya watoto  ambao hulazimika  kuchanganywa na wakubwa, kina mama hujifungua kwa kutumia mwanga wa simu ya tochi pia uhaba wa maji upo.
“ Kijiji hiki kinahudumia zaidi ya watu 21,000, awali kulikuwepo na sola ambayo ilikuwa ikisaidia  kurahisisha huduma mbalimbali kwa wagonjwa lakini ilikwisha ibiwa na sasa hakuna sola vifaa vya kupimia  maradhi mbalimbali ikiwemo malaria hakuna ,wodi ya kulaza watoto  hakuna inawalazimu kuwachanganya na wakubwa hata  wenye magonjwa ya kifua kikuu na kuhara”alisema .
Naye  mkuu wa kituo hicho Dkt  Saimon Wilson alisema   vifaa vya kupimia baadhi ya maradhi vipo   ila kuna wengine wagonjwa hulazimisha  kupata vipimo vyote vingine havipo ila kwa upande wa  kupima malaria kipimo kipo, suala la kujifungulia tochi  ya simu sio kweli bali wanatumia taa ikiwa sola iliyopo haina nguvu na huzimishwa ifikapo  saa tano usiku.
"Kituo hiki  kinakabiliwa na  changamto ya maji na nishati ya umeme,  suala la sola kuibiwa siwezi kulizungumzia   mimi nilikuta  sola iliyopo  na  inatumika  mpaka sasa ni hii nayo haina nguvu huwashwa  na kuzimishwa saa tano usiku ,tunatumia taa za kawaida,pia wagonjwa kwa siku ni zaidi ya 80",aliongeza.
Diwani wa kata hiyo   Joseph  Budonho  alisema kuwa  kweli  kituo hicho cha afya  kina changamoto ya ukosefu wa  nishati ya umeme na maji  ila tatizo hilo linashughulikiwa   ikiwa tayari nyaya za umeme zimekwisha wekwa   isitoshe kuondoa  tatizo la maji lililopo, kuhusu sola  ilikuwepo  zamani lakini iliibiwa na kesi bado ipo mahakamani.
Chanzo-Kareny Blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments