Ukatili!!! MTOTO ALIYETAKA KULAWITI ACHOMWA MOTO SEHEMU ZA SIRI,MHUSIKA ASHIKILIWA NA POLISI

BADO tatizo la unyanyasaji dhidi ya Watoto limeendelea kukua kwa kasi, Wilayani Babati Mkoani Manyara, ambapo Jeshi la Polisi Mkoani humo, linamshikilia Mama wa kambo wa Mtoto wa kiume, anayedaiwa kutaka kumlawiti mtoto wake na kisha kumchoma na kijinga sehemu za siri.  

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani humo, Mussa Marambo alithibitisha kukamatwa kwa mwanamke huyo mkazi wa Magugu, ambapo alisema tukio hilo lilitokea juzi Machi 9, mwaka huu saa 12 jioni, wakati watoto hao wakicheza mchezo wa kujificha na kumtaja mtoto anayedaiwa kufanya kitendo hicho kuwa ni Joakim Mkumbo (9).  

Alimtaja mwanamke anayeshikiliwa kuwa ni Lydia Mkumbo (39), anayedaiwa kumchoma sehemu za siri Mtoto wake wa kambo, kwa tuhuma za kutaka kumlawiti mtoto wake, ambapo Jalada la mtuhumiwa huyo limepelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali akisubiri kufikishwa Mahakamani, huku mlalamikaji akiwa amelazwa katika Kituo cha Afya cha Magugu akiendelea kupata matibabu baada ya afya yake kuelezwa kuwa ni mbaya.  

“Aliumizwa sehemu za siri kwa kumchoma na kijinga cha moto, uchunguzi wa wali umeonyesha kuwa, chanzo cha tukio hilo kinaweza kuwa Mama huyu alihisi huyo kijana alikuwa na nia ya kutaka kumlawiti mtoto wake” alisema Marambo.  

Tukio hili ni la pili kutokea Wilayani humo, ambapo juma lililopita Mwanafunzi wa Kike anayeishi na Baba yake mzazi, Mwanafunzi wa darasa la Kwanza katika Shule ya Msingi Darajani, mwenye umri wa miaka (10) alimtuhumu wazi wazi Baba yake mzazi kwa Mwalimu wake kuwa amekuwa akimbaka mara kadhaa nyakati za usiku licha ya kutoa taarifa kwa ndugu wa Mama yake bila kuchukuliwa hatua yoyote.  

Kufuatia kutokea kwa matukio kadhaa kama hayo, Kamanda huyo amewataka wananchi kuacha tabia ya kunyamazia matukio kama hayo, na hivyo kuwataka wananchi kushirikiana na Serikali za Mitaa kutoa taarifa hizo mapema. 

      Na Dotto Mnzava-Manyara

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post