Zikiwa zimesaria siku chache ili kufikia kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani siku ya Jumamosi wiki hii tarehe 8,mwezi huu,wakazi wa Shinyanga wameombwa kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho hayo ambayo katika wilaya ya Shinyanga yatafanyika katika uwanja wa michezo shule ya msingi Nhelegani kata ya Kizumbi kuanzia saa tatu asubuhi.
Akizungumza leo katika kikao cha maandalizi ya sherehe hizo kilichofayika katika ukumbi wa ofisi ya afisa matendaji kata ya Ngokolo mjini Shinyanga,mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya sherehe hizo katika wilaya ya Shinyanga bwana Mtinga Masatu ambaye ni mwenyekiti wa mtandao wa asasi za kiraia katika manispaa ya Shinyanga-SHIMUNGONET amesema ni vyema wananchi wote wanawake kwa wanaume wakahudhuria maadhimisho hayo.
Masatu amesema mgeni rasmi katika maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa mkuu wa wilaya ya Shinyanga Bi Anna rose Nyamubi na kuongeza kuwa siku hiyo kutafanyika maandamano kuanzia ofisi ya mtendaji kata ya Kizumbi kuelekea kwenye uwanja wa Michezo wa shule ya msingi Nhelegani.
Masatu ameongeza kuwa katika kuadhimisha siku ya wanawake duniani katika manispaa ya Shinyanga,mbali na kufanyika kwa maandamano hayo pia kutakuwepo na shughuli mbalimbali kama vile maonesho ya bidhaa za wanawake wajasiriamali,upimaji hiari wa VVU,burudani na mambo kadha wa kadha ambayo wamejipanga vyema katika kuhakikisha siku hiyo inafana kweli kweli.
Ametumia fursa hiyo kuwaomba wakazi wote wa Shinyanga
kujitokeza kwa wingi siku hiyo na kuongeza kuwa wale watakaopata nafasi
basi wawahi eneo la benki ya NBC mjini Shinyanga kusubiri usafiri wa
kuwapeleka eneo la tukio kuanzia saa moja na nusu asubuhi hadi saa mbili asubuhi
Aidha mwenyekiti huyo SHIMUNGONET amesema ujumbe wa siku ya wanawake mwaka huu ni "Chochea mabadiliko kuleta usawa wa kijinsia".
Social Plugin