GEITA WAMTAKA WAZIRI MKUU PINDA KUINGILIA SAKATA LA KIJIJI KUTOSAJILIWA

 
Wananchi wa kijiji cha Mgusu kilichopo wilayani Geita mkoani Geita wameilalamikia kamati ya madiwani walioenda kuangalia mgawanyo wa rasilimali za halmashauri na kuibua hoja ya kuwa kijiji chao hakina usajili na kumwomba waziri mkuu aingilie kati suala hilo mapema iwezekanavyo.


Kijiji cha Mgusu kilichopo katika kata ya Mtakuja wilayani Geita kimebainika kuwa hakina usajili kama kijiji licha ya wakazi wa kijiji hicho kufahamu kuwa kijiji chao kina usajili kilichoupata tangu 2009 chini ya mbunge aliyekuwepo Ernest Mabina.

Sintofahamu hiyo imeibuka hivi karibuni katika kamati ya maridhiano baina ya halmashauri ya mji wa Geita na halmashauri ya wilaya ya Geita mara baada ya kugawana eneo la utawala na rasilimali zilizokuwa zinamilikiwa na halmashauri mama ya wilaya.

Kamati hiyo iliyokuwa na taarifa ya mapendekezo juu ya mgawanyo wa mapato yatokanayo na shughuli za uchimbaji wa dhahabu katika mgodi wa Geita Gold Mine (GGM) iliyowasilishwa kwenye baraza la madiwani tar 16.7.2012 ilibaini katika hadidu za rejea za kutambua maeneo/mipaka ya leseni ya uchimbaji wa dhahabu special mining license(SLM 45/99).

Aidha masuala muhimu yaliyobainika baada ya tume kukamilisha zoezi la tathmini ni katika kifungu cha 3.4 ambacho kinaeleza kuwa kijiji cha Mgusu kimo ndani ya hifadhi ya msitu wa Geita (Geita Forest Reserve) na hakijasajiliwa.

Aidha kifungu namba 3.8 kinasema....

 “Pia tume ilibaini vijiji vilivyomo ndani ya leseni ya uchimbaji(SML) kama ifuatavyo, Nyamalembo,Mtakuja,Katoma,Mgusu(kijiji hiki hakina usajili)’’

Kifungu namba 3.1 nacho kinasema... “Mipaka ya leseni ya GGM ya uchimbaji wa dhahabu (SML 45/99) imo ndani ya hifadhi ya msitu wa Geita (Geita Forest Reserve –GN 10 ya mwaka 1953 ambapo mmiliki wake ni Wizara ya mali asili na utalii kupitia wakala wa msitu (Tanzania Forest Agency)’’.

Nukuu hizi zote zinaonyesha kuwa kamati hiyo ilibaini kijiji cha mgusu hakijasajiliwa na kinakaliwa na watu ambao wako kwenye hifadhi ya msitu na wanafanya kazi za uchimbaji kwenye eneo la hifadhi ambapo pia ni leseni ya mgodi wa GGM special mining license ya mwaka 1953 hivyo basi hawatambui uwepo wa kijiji hicho kisheria.

Mwenyekiti wa wachimbaji wadogo wadogo Mhoja Kiyuga ambaye alikuwa mwenyekiti wa kijiji hicho cha Mgusu alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema kijiji hicho kimesajiliwa kisheria.

“Ninasema kuwa kijiji kimesajiliwa tangu 2005 na Jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa sheria namba 7 ya mwaka 1984 na kupewa namba MZ.KIJ/734 tarehe 8 julai 2005 na kipo katika kata ya Mtakuja wilaya ya Geita Mkoa wa Mwanza kipindi hicho na kilisainiwa na B.B. Claudio msajili wa vijiji.

Bwana Mhoja aliongeza kuwa eneo  hilo ni hifadhi na tena sio eneo la GGM.

 “Sisi tumepewa leseni  viwanja 20 vya Saccos yetu kwa ajili ya kuchimba wachimbaji wadogo wadogo, na tulipewa leseni hizo na naibu waziri wa nishati na madini Stephen Masele  mwaka 2012 hivyo huwezi kusema kuwa ni eneo la GGM ama ni hifadhi tena kwa ushahidi wote wa kiserikali niliokutajia hapo mwandishi na tunalipa mapato yote na mrahaba kama sheria ya madini inavyosema hata ukienda ofisi ya madini’’ alisema Mhoja.

Kwa upande wa Michael Malebo ambaye ni mchimbaji mdogo mdogo katika kijiji hicho cha Mgusu amesema kuwa licha ya maeneo ambayo wanayafanyia kazi hata GGM wana maeneo yao tofauti na sehemu walizopewa wananchi lakini bado athari za kimazingira zinawaathiri sana mfano ulipuaji wa maeneo mbalimbali.

Baadhi ya wananchi walioongea na waandishi wa habari hizi wamesema kuwa wanafikiria kuishitaki kamati hiyo ambayo iliundwa kwa ajili ya kutengua usajili wa kijiji hicho.

 “Hata waziri mkuu Mizengo Pinda alishawahi kufika hapa kwa nyakati tofauti tofauti akijua ni kijiji leo hii wanatuambia tunakaa kwenye hifadhi na leseni ya GGM kwa hiyo GGM anaruhusiwa kukaa kwenye hifadhi ila wananchi hawarusiwi? “,alihoji mmoja wananchi hao.

“Kama tulishapewa na leseni za uchimbaji 20 na serikali hiyo hiyo ,ina maana hata naibu waziri wa madini alikuwa hajui au kuna kitu gani wanachokitafuta hawa watu?”,mwingine alihoji.

Mmoja wa wajumbe waliokuwa kwenye kamati hiyo ambaye si msemji wa kamati alisema kuwa....

 “sisi tulimaliza kazi yetu ya kugawana raslimali za halmashauri na hayo yote yalikuwa yakifanyika kwa mujibu wa hadidu za rejea tulizopewa kwa hiyo tulimaliza kazi sisi”.

Aliongeza kuwa hali hiyo inaweza kuleta mgongano kati ya wananchi wanaoishi kijiji hicho na baadhi ya viongozi ambao walikuwemo kwenye kamati hiyo huku wakijua kuwa ni kijiji kilichosajiliwa lakini wao wanasema kuwa hakina usajili na wameenda mbali zaidi wakitaka waziri mkuu aingilie suala hili ili wananchi wajue hatma yao ya makazi ndani ya kijiji hicho.

Na Valence Robert-Geita


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post