ALIYETUMIA JINA LA NAPE NNAUYE KUTAPELI WATU HUKO GEITA,AFUNGWA JELA MWAKA 1



 
Mahakama  ya wilaya ya Geita imemhukumu kwenda jela Selemani Nkwenda(36) mkazi wa mseto mjini Geita baada ya kutumia jina la katibu wa siasa na uenezi CCM Nape Nnauye kutapeli watu kipindi cha uchaguzi wa chama 2012.

Akisoma mashtaka hayo mbele ya hakimu wa mahakama hiyo Zabroni Kesase ,wakili wa serikali Janet Kisabo alisema Selemani Nkwenda alitenda kosa hilo mnamo tarehe 5 na 19 mwaka juzi akiwa eneo la Mseto  ambapo alimpigia simu Peter Mwininga kwa namba 0767768464 na kujitambulisha kuwa yeye ni Nape Nnauye na kumwambia kuwa atampigia baadae waongee zaidi.

Aidha katika kosa la pili mtuhumiwa mnamo tarehe 19 mwaka juzi alimpigia simu kwa namba hiyo hiyo na kumwambia amtumie pesa kiasi cha shilingi milioni moja na laki tano huku akidai yeye yuko Dodoma makao makuu ya chama na atajitahidi jina la Mwininga alirudishe kwa vile alikuwa anagombea nafasi ya mwenyekiti wa vijana mkoa wa Geita.

Baada ya kumaliza kusoma mashitaka hayo wakili huyo aliiomba mahakama itoe adhabu kali dhidi ya mtuhumiwa ili liwe fundisho kwa wengine wenye nia ya kutaka kutenda kosa kama hilo katika jamii.

Hakimu wa mahakama hiyo Zabroni Kesase aliyekuwa anaiskiliza kesi hiyo baada ya kujiridhisha na pande zote za mtuhumiwa na mlalamikaji  huku ushahidi ukijitosheleza bila mashaka yoyote ,alitoa hukumu ya kifungo cha mwaka mmoja ikiwa ni kila kosa ni kutumikia kifungo cha miezi sita na kwa makosa mawili anatumikia kifungo cha mwaka mzima.

Imeelezwa kuwa mtuhumiwa tangu mwaka juzi katika uchaguzi wa ndani wa chama cha mapinduzi uliokuwa unafanyika kote nchini alitumia mwanya huo kuweza kutapeli watu mbalimbali mkoani Geita kabla hajakamatwa na kutiwa hatiani akitumia jina la katibu siasa, itikadi na uenezi wa chama cha mapinduzi taifa Nape Nnauye.

Na Valence Robert-Geita

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post