YULE MTUME ALIYETABIRI MWISHO WA DUNIA AMEFARIKI DUNIA


DUNIAKUISHA
Mtume wa Kanisa la World Message Last Warning nchini Uganda ambaye alitabiri kwamba mwaka 2000 utakuwa mwisho wa dunia, Wilson Bushara (53) amefariki dunia.
Bushara ambaye alivuta vyombo vingi vya habari alipotabiri na kusisitiza kwamba mwisho wa dunia utakuwa Juni 30 mwaka 1999 na kushawishi waumini wake kuuza mali zao na kununua nafasi zao mbinguni alifariki asubuhi ya jana.
Alitabiri na kusisitiza kwamba dunia itafikia mwisho wake kabla ya kuingia kwa milenia mpya, ambayo ilikuwa ni mwaka 2000.
Hata baada ya tarehe hiyo aliyoitaja kupita bila tukio hilo kutokea, Bushara alikimbilia mafichoni baada ya polisi kuvamia kambi yake ya maombi ya Bukoto iliyokuwa huko kwenye Wilaya ya Luweero Jimbo la Nakaseke Septemba 18, 1999.
Bushara anatambulika kuwa ana ushirikiano na kiongozi mwingine wa kundi la kidini, Joseph Kibwetere ambaye aliwashawishi waumini wake zaidi ya 1000 kujichoma moto kanisani Machi 17, 1999.
Hata hivyo aliamua kukataa kuwa na ushirikiano na Kibwetere pamoja na kuwa na ushahidi wa picha walizopiga kwenye matukio kadhaa wakiwa pamoja.
Bushera pamoja na baadhi ya waumini wake ambao wengi walikuwa wakifanya kazi za kuuza maziwa na uhudumu kwenye hoteli wote walikimbilia wilayani Busia ambapo walijificha baada ya kusikia taarifa kwamba polisi walikuwa wakitaka kuwakamata.
Alioa wake tisa aliokuwa akiishi nao kwa pamoja, mmoja kati yao akiwa binti wa miaka 15. Miaka 10 baadaye, yaani mwaka 2011 Bushara aliibuka na kutabiri kwamba dunia inaelekea kufikia mwisho wake siku za karibuni na kuanza kugawa kadi za mwaliko kwa waumini wake, kwa ajili ya tafrija maalumu ya “karamu ya mwisho” ambazo kila moja iliuzwa kwa Sh23,000 za Uganda.
Aliwaeleza wafuasi wake kwamba ishara za mwisho huo wa dunia ziko wazi ikiwemo miale mikali ya radi na milipuko ya volcano wanayoishuhudia kwa mwaka huo ndiyo uthibitisho kwamba dunia imefikia mwisho.

 Kwa kusisitiza, aliwahakikishia kwamba wale watakaokuwa wamenunua kadi hizo ndio watakaopata fursa ya ‘kunyakuliwa’ moja kwa moja kwenda mbinguni na wale ambao hawatakuwa wamezipata, wataishia kwenye moto wa jehanamu.
Kwa wakati huu, Bushara alikuwa makini akikataa kutaja tarehe rasmi ya mwisho huo wa dunia aliokuwa akiutabiri.  Bushara amefariki huku akikabiliwa na mashtaka kadhaa mahakamani, ikiwemo kufunguwa kanisa lake ambalo lilipigwa marufuku.
Mei mwaka jana alishtakiwa kwa ulaghai na kuitisha mkusanyiko usiokuwa halali kisheria, kisha kushikiliwa kwenye gereza la Luzira na hatimaye kuachiwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post