WABUNGE WA BUNGE MAALUM LA KATIBA WATAKIWA KUWEKA MASLAHI YA TAIFA MBELE


Wabunge wa bunge maalumu la katiba wameshauriwa kuweka mbele maslahi ya taifa badala ya kutanguliza itikadi ya vyama vyao vya kisiasa hali inayoweza kuchangia kushindikana kupatikana kwa katiba mpya nchini. Ushauri huo umetolewa juzi na wajumbe wa asasi zinazojihusisha na utoaji wa huduma za msaada wa kisheria mkoani Shinyanga wanaohudhuria mafunzo ya siku nne mjini humo yaliyoandaliwa na Mtandao wa watoa huduma wa msaada wa kisheria (TANLAP) kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa kazi zao. 

Wajumbe hao walisema ni muhimu wabunge wa bunge maalumu la katiba wakaingia bungeni wakiwa na mshikamano mmoja kwa maslahi ya nchi kwa ajili ya kujadili vifungu vilivyomo ndani ya rasimu ya pili ya katiba bila kutanguliza matakwa na maono binafsi kutoka ndani ya vyama vyao. 

Walisema iwapo wabunge hao hawataelewana ni wazi mchakato mzima wa kupatikana kwa katiba mpya utavurugika na inaweza kuwa moja ya sababu ya nchi kuingia katika vurugu kubwa ambayo haipaswi kutokea iwapo busara itawekwa mbele katika siku zote 70 za kujadili rasimu hiyo. 

Mmoja wa wawezeshaji katika mafunzo hayo kutoka Shirika la PACESHI Shinyanga, John Shija alisema moja ya mambo ya msingi ambayo wabunge hao wanapaswa kuzingatia ni suala la haki za kibinadamu kuhakikisha yale yote yaliyopendekezwa na watanzania yanakuwemo ndani ya katiba mpya. 

“Yapo mambo mengi ya msingi yanayopaswa kuzingatiwa na wabunge wetu hawa hasa suala la haki za binadamu, kwa mfano ibara ya 10 ndani ya rasimu inazungumzia suala la haki za kisheria, ibara hii ni muhimu sana, na sisi watoa huduma za msaada wa kisheria tuhakikishe haiondolewi,” 

“Kutokuwepo kwa ibara hii kunaweza kuchangia sehemu kubwa ya jamii hapa nchini wakose haki zao za kisheria kwa mujibu wa katiba, hivyo tuhakikishe wabunge wetu wanaipitisha badala ya kuiondoa, na tunawaomba waitetee rasimu hii bila kujali itikadi ya vyama vya siasa wala ushabiki wa aina yoyote ile,” alieleza Shija. 

Kwa upande wake mmoja wa wanasheria kutoka TANLAP, George Molel alisisitiza suala la wabunge wa bunge la katiba kuzingatia zaidi yale yaliyopendekezwa na watanzania na kwamba wanachopaswa kufanya ni kuyaboresha zaidi badala ya kupunguza au kuingiza maoni yao binafsi ambayo hayana baraka za wananchi wala Tume ya Jaji Joseph Warioba. 

“Tunachowaomba wabunge wetu hawa wa bunge la katiba wawe makini sana, wasiongozwe na matakwa ya vyama vyao vya siasa, tunataka wafanye kazi ambayo wametumwa na watanzania, waboreshe rasimu ili iweze kukubalika na watanzania wote, wasiingize rasimu zao za pembeni kutoka ndani ya vyama vyao,” alisema Molel. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post