Unyama!! BABA AMBURUZA MTOTO WAKE KWENYE PIKIPIKI MTAA MZIMA,BAADA YA KUGOMA KWENDA SHULE


Mtoto Anastazia Jumanne akiwa amefungwa kwenye pikipiki

Mtoto Anastazia Jumanne (12) ambaye ni mwanafunzi wa shule ya msingi Mkoani wilayani Geita mkoani Geita amefanyiwa ukatili wa kutisha baada kufungwa kamba na baba yake mzazi kisha kumfunga kwenye pikipiki na kuanza kumburuza mtaa mzima kwa kutumia pikipiki hiyo.

Tukio hilo la kusikitisha limetokea jana majira ya sa tatu asubuhi katika mtaa wa Mkoani ambapo inadaiwa kuwa binti huyo anayesoma darasa la nne katika shule hiyo alikataa kwenda shuleni kitendo ambacho kilimkasirisha baba yake aitwaye Jumanne Nkoyogi ambaye pia ni mfanyabiashara wa samaki mjini Geita.

Mashuhuda wa tukio hilo baada ya kuona asubuhi majira ya saa 3 akiburuzwa huku amefungwa kwenye pikipiki walianza kupiga makelele na kukusanyana kwa lengo la kumkamata bwana huyo aliyekuwa anafanya unyama huo.
 Baada ya kumtia mikononi walimpeleka kwenye ofisi ya sungusungu iliyopo Ihayabuyaga kata ya Kalangalala na kufungiwa humo kwa usalama wake.

Akizungumzia tukio hilo katibu wa sungusungu kata ya Kalangalala aliyempokea mtuhumiwa huyo Abel Richard alisema tukio hilo liliwafanya wananchi kujaa hasira kali dhidi ya mzazi huyo na kutaka kumpiga hadi waue lakini baada ya yeye kuwasiliana na polisi,polisi walifika haraka na kumchukua hadi kituoni kwa usalama wake.

Afisa upelelezi wa mkoa wa Geita Simon Pasua amekiri kuwepo kwa tukio hilo na kusema kuwa mtuhumiwa anashikiliwa na jeshi la polisi hadi sasa kwa upelelezi zaidi.

Na Valence Robert-Geita

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post