KONDA AFARIKI DUNIA AKIWASAIDIA WATU KUVUKA BARABARA

Kondakta Remfan Mushi (30), mkazi wa Tegeta Wazo, amefariki dunia juzi jijini Dar es Salaam baada ya kugongwa na gari alipokuwa akiwasaidia watembea kwa  miguu kuvuka barabara.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, alisema jana kuwa ajali hiyo ilitokea saa 10 jioni eneo la Boko Califonia katika barabara ya Bagamoyo.

Alisema  kabla ya tukio hilo, dereva wake aliyekuwa akiendesha gari T 901 BSM Coaster alisimamisha gari kwenye kivuko (Zebra Cross), ili kondakta wake ashuke na kuwaruhusu watembea kwa miguu kupita.

Kamanda Wambura alisema baada ya kondakta huyo kushuka, aligongwa na gari T 865 BQA Fuso Tipper iliyokuwa ikiendeshwa na dereva ambaye hakufahamika na kufariki dunia papo hapo.

Wambura alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva wa Fuso aliyekuwa akitokea Bagamoyo kuelekea Tegeta kushindwa kusimama kwenye kivuko cha watembea kwa miguu.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Mwananyamala na hakuna aliyekamatwa. Polisi wanaendelea kumsaka dereva aliyesababisha ajali hiyo.

Katika tukio jingine, mkazi wa Kimara Bonyokwa, John Mloa aneyekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 45 hadi 50, amefariki dunia ghafla baada ya kuanguka.

Tukio hilo lilitokea juzi, saa 4 asubuhi baada ya mtu huyo  kuanguka na kuzirai. Alifariki dunia akiwa njiani akipelekwa Hospitali ya Tumbi, na sababu za kifo bado hazijafahamika.
Via>>Tanzania daima

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post